SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 28 Julai 2016

T media news

KWA NINI MKE WA MTU ANAKUWA MKE WA WATU


HATUNA budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha tena katika uwanja wetu maridhawa wa kupeana darasa la uhusiano. Siku zote ukikubali kupokea na kufanyia kazi yale tunayopeana kila Jumamosi kupitia safu hii.



Mada yetu iliyohusu mke wa mtu kuwa mke wa watu. Nilieleza namna ambavyo mke wa mtu anavyoweza kuangukia katika dmbwi la kuwa mke wa watu kwa sababu ya kukosa umakini.

Anashindwa kujua kwamba kama mke wa mtu anapaswa aishi vipi na ndugu, jamaa na marafiki ili asitoe mwanya wa watu kumfanya mke wa watu.Tumalizie mada hii kwa kutazama mazingira na vichocheo vinavyowasababisha mke wa mtu ageuke kuwa mke wa watu. Mbali na kujua vichocheo hivyo, pia tutapata kujua mbinu mbalimbali za kuepukana na tatizo hili:

UMBALI

Unapokuwa umeolewa moja kwa moja utakutana na mashemeji utakutana na marafiki wa kiume kama vile ulivyokuwa hujaolewa. Suala la msingi hapa ni mabadiliko. Unatakiwa kubadilika ili usiweze kutoa mwanya wa vishawishi.

Kama mtu ni shemeji yako, muwekee mipaka yake. Usikae naye kama vile unavyokaa na mumeo. Hata kama yeye ataleta ukaribu, wewe ndiyo unatakiwa kuweka mipaka. Ukiruhusu akukaribie, utarusu akushike na baadaye anaweza kufikia hatua ya kula tunda analokula kaka yake.

Epuka mazoea yasiyo kuwa na tija. Mazoea ndiyo yale ndiyo yanaletaka ‘shemeji shemeji huku mwazima taa.’Utani unaanzaga taratibutaratibu, unaota mizizi na baadaye mnafanya kweli. Mtu ambaye si mume wako, hakikisha hakukaribii. Mpe salamu, zungumza naye lakini asiwe karibu kupindukia.


KIPAUMBELE

Kama binadamu, wanawake nao wana matamanio. Anaweza kuvutiwa na kitu fulani kutoka kwa mtu fulani ambacho pengine mumewe hana. Ataanza kwa kuvutiwa, baadaye atataka kuonana naye na mwishoni wanajikuta ni wapenzi.

Mke anayejiheshimu hawezi kumpa kipaumbele mwanaume mwingine yeyote kwa kigezo chochote. Mumewe ndiyo wa kwanza katika hali yoyote. Hata kama mwanaume fulani ana fedha kuliko mumewe, ana sifa ya ziada kuliko mumewe, anapaswa kusema mumewe ndiyo zaidi.

Kamwe hampi kipaumbele mwanaume mwingine. Ukimwambia mwanaume mrefu mzuri, hata kama mumewe ni mfupi atakwambia mumewe ni mrefu kuliko wanaume wowote. Hivyo ndivyo inavyotakiwa.

Atakwambia ameridhika na urefu wa mumewe ndiyo alioupendea. Hilo ndilo penzi la dhati.

KUTOTOA SIRI

Mwanamke ambaye hana heshima hutoa siri za ndani. Kama mumewe ana tatizo fulani, analiweka wazi kwa marafiki wa kiume wa mumewe pasipo kujua anatoa mwanya wa kutongozwa. Wanaume wajanja wanasoma udhaifu, wanakutimizia na furaha yako inaendelea kuwepo bila ya mumeo.

Tunza siri. Kama kuna tatizo la faragha, jaribu kuzungumza na mwenzako ili mtafakari kwa pamoja kuhusu suluhu. Kama ni tatizo linaloweza kutibika hospitali, nendeni mkapate ushauri wa kitabibu.

Ni matumaini yangu endapo utayazingatia hayo tuliyoyadili, hakikaka huwezi kuwa mume wa watu bali utakuwa mume wa mtu mmoja ambaye mtaishi kwa upendo, amani na furaha.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!