SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 29 Julai 2016

T media news

Jicho La 3: MO, KARIBU SANA SIMBA SC, NIONE TIMU YA NDOTO ZANGU…


Na Baraka Mbolembole

Alhamisi hii rais wa klabu ya Simba SC, Evance Aveva alisema kwamba ni wanachama pekee wa klabu hiyo ambao watatoa mwelekeo mpya wa klabu, kutoka mfumo wa sasa wa kutegemea wadhamini hadi kuwa kampuni ambayo itauza hisa zake huku wanachama wa klabu wakiwa sehemu ya wamiliki.

Kiukweli kwa mara ya kwanza nimependezwa na mtazamo wa Aveva na amezungumza akiwakilisha walio wengi ambao wamekuwa na ndoto ya kuiona timu yao ikipiga hatua kiuchumi na kimpira ndani na hata nje ya bara la Afrika.

Leo, Ijumaa ‘mwanzilishi’ wa wazo hilo, tajiri mkubwa Afrika, Mohammed Dewji pia amewasisitiza wanachama kuelekea mkutano wao wa mwaka siku ya Jumapili kukubaliana na mpango huo huku akiahidi kuisaidia klabu usajili wa mabadiliko hayo (kutoka mfumo wa sasa hadi kuwa kampuni).

Kukubali kwa Aveva sidhani kama kuna shinikizo lolote amelipata bali naamini miaka yake miwili madarakani kama rais wa klabu hiyo amejifunza mengi na atakuwa ametazama mwelekeo wa mbali zaidi wa klabu hiyo. Aveva hajashindwa, lakini miaka miwili kama rais wa klabu hata yeye amekubali na ameona kuna ulazima wa klabu kujiendesha katika mfumo wa soko la hisa.

MO aliahidi kununua asilimia 51 ya hisa huku zile 49 zikibaki kwa wanachama hivyo Simba tayari wana mtu wa kuwapeleka kule ambako kila mwanasoka anataka kuona klabu hiyo iliyoliyoanzishwa mwaka 1936 ikifika. Lakini upande wangu naamini kila mabadiliko ni hatua-inaweza kuwa hatua ya kusonga mbele au kurudi nyuma.

Wanachama wa Simba wanapaswa kutumia nafasi waliyopewa ya kufanya mabadiliko kwa umakini mkubwa.

Ni vema wangetumia mkutano ujao kwanza kujadili kwa mapana faida/hasara. Kama, MO anaamini kuwa mabadiliko hayo si jambo la siku moja, basi wanachama wa Simba ni vizuri ‘kupembua’ mambo kwa umakini zaidi moja baada ya jingine kisha mkutano wao mkuu uwe wa kufikia maamuzi.

‘Ugumu wa maisha ndiyo kipimo cha akili,’ na wanachama wa Simba watumie misimu yao minne bila taji na kuigeuza kufeli kwao kuwa njia ya kufanikiwa. MO anataka kuisimamisha timu anayoipenda na kuishabikia.

Kama ataichukua timu hiyo, naamini Simba itakuwa na uwanja wake wa kisasa ndani ya michache ijayo na itakuwa mbali sana kiuchumi, ila ni lazima kwanza wanachama wapewe muda wa kujadili ili kujiridhisha na mwelekeo wanaoutaka.

Naamini chini ya mfumo mpya nitaiona ‘Simba ya ndoto zangu’, MO karibu sana Simba SC, nione timu ya ndoto zangu,  ila wape wanachama nafasi ya kutafakari.