Msanii wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini, Emmanuel Elibariki maarufu Nay wa Mitego amesema kuwa anajiona akiachana na muziki na kuanza kufanya shughuli nyingine kutokana na kushindwa kubadili mfumo wa muziki wake kama ambavyo ametakiwa kufanya hivyo na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakishirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Nay wa mitego amefikia hatua ya kusema hayo, ikiwa ni muda mfupi tu tokea alipoitwa na Wizara inayosimamia mambo ya sanaa ikimtaka abadili maudhui ya baadhi ya nyimbo zake alizozitoa, pamoja na kufanya marekebisho kwa baadhi ya nyimbo hizo.
Nay amesema kuwa kubadili mfumo wa muziki wake ni sawa na kuharibu sanaa yake, jambo ambalo linamsababishia hasara kila wakati, nyimbo zake zinapofungiwa.
“Sioni nikibadilisha mfuno wa mashairi kwa sababu nitakuwa nimeenda kuharibu sanaa yangu. Labda najiona nikienda kuachana na muziki na kuamua kufanya shughuli zingine. Naona kama wengine wamekuwa ni chambo tu. Nia kubwa imekuwa ni kwangu kwa sababu kiukweli kabisa ukiangalia nyimbo zilizowekwa kwenye list, nyingi zimeshapitwa na wakati na tayari nyimbo zilishavuma, watu walishafanyia biashara, washrudisha hela zao, lakini wimbo mpya ni mmoja tu wa mikono juu ambao nimeutoa wiki mbili zilizopita. Video ndio kwanza ina ‘one week’. SAsa kila siku nitakuwa napata hasara, naona tu niangalie ustaarabu wa kufanya ishu nyingine,” alisema Nay wa Mitego katika mahojiano kwa njia ya simu na Shirika la Utangazaji la uingereza (BBC).
Pamoja na kuwa na mpango wa kuachana na muziki, Nay alisema kuwa atafikisha ujumbe kwa mamlaka husika ili waufanyie kazi ikiwa ni kwa lengo la kuokoa sanaa ya Tanzania na muziki uendelee kusonga mbele.
“Lakini sitaacha hivi hivi. Kuna kitu nitazungumza kwa ajili ya sanaa yetu kwa sababu imeniokoa hata mimi. labda ningekuwa meizi, ningekuwa nimeshauawa, lazima niongee kitu kwa ajili ya sanaa yetu, viongozi wenye mamlaka za juu ambao watasikia na wataona, watalifanyia kazi kwa ajili ya kuokoa saanaa yetu, muziki wetu uendelee kusonga..” aliongeza Nay.
Hapo jaba, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza akiongea na waandishi wa habari alisema kuwa, wizara yake imempa onyo Nay wa Mitego kutokana na kutoa nyimbo ambazo zina maudhui yaliyo kinyume na maadili.
Kabla ya hapo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitangaza kuzifungia nyimbo 14 za wasanii mbalimbali hapa nchini, ambapo nyimbo tatu za msanii Nay wa Mitego zimefungiwa kupigwa katika vituo vya redio na runinga kutokana na kuwa na maudhui yanayokiuka maadili ya nchi.