Na Mahmoud Rajab
Dejan Lovren, Vincent Kompany, Morgan Schneiderlin na Diego Costa wote kwa pamoja hawatoonekana katika michunao ya Euro mwaka huu nchini Ufaransa.
Wachezaji wengi wenye majina makubwa wanaocheza ligi ya England watakuwa na timu zao kwenye EURO mwaka huu.
Mataifa yote 24 yakayokuwa yakiwania ubingwa huo, yamechagua vikosi vyao kwa ajili ya michuano hiyo, ambayo itaanza June 10.
Hata hivyo , kuna baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa ambao watakosekana katika EURO ya mwaka huu baada ya ama kutokuchaguliwa kutokana na majeraha au viwango vyao kutowaridhisha makocha wao.
Mtandao wa Sky Sports umekuja na first eleven ya wachezaji hao watakaokosa EURO mwaka huu.
Mlinda lango: Rob Elliot (Jamhuri ya Ireland)
Rob Elliot alipata majeraha wakati wa mchezo wa kirafiki.
Kipa huyu wa Newcastle United atakosa mashindano hayo kutokana na kupata majeraha katika mchezo dhidi ya Slovakia mwezi March mwaka huu.
Beki wa kulia: Kurt Zouma (Ufaransa)
Kurt Zouma atakosa kutokana na majeraha. Beki huyu wa Chelsea aliumia katika mchezo dhidi ya Man Utd ambao uliisha kwa sare.
Beki wa kati: Vincent Kompany (Ubelgiji)
Vincent Kompany aliumia wakati timu yake ya Man City alipokuwa ikipambana na Real Madrid katika nusu fainali ya Champions League. Atakuwa nje kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Beki wa kati: Dejan Lovren (Croatia)
Dejan Lovren alikuwa shujaa wakati Liverpool ikiiupa nje Borussia Dortmund katika nusu fainali ya EUROPA.
Kuachwa kwake kumewashangaza wengi sana, Lovren hajajumuishwa katika kikosi cha cha Croatia baada ya kutochaguliwa na kocha wake Ante Cacic. “Kuchezea timu ya taifa kunahitaji kuwa katika kiwango bora na moyo mkubwa wa kujitolea iwe ndani ya klabu au timu ya taifa. Tunataka kufanya timu yetu kuwa yenye ushindani. Sijafunga mlango kwa Lovren milele, anaweza kurudi siku moja endapo atatambua kwamba anahitajika kucheza kwa ajili ya timu”, Cacic alisema.
Beki wa kushoto: Chris Brunt (Ireland ya Kaskazini)
Chris Brunt aliumizwa na Wilfried Zaha. Brunt aliumia wakati timu yake ya West Brom ikishinda mabao 3-2 dhidi ya Crystal Palace.
Midfield: Juan Mata (Hispania)
Juan Mata hayupo katika kikosi cha Hispania kutokana na kiwango chake kushindwa kumshawishi kocha wake Vicente del Bosque.
Midfield: Santi Cazorla (Hispania)
Santi Cazorla akicheza timu ya Arsenal chini ya miaka 21 baada ya kupona majeraha yake aliyopata kwenye mchezo dhidi ya Norwich.
Akiwa amecheza mchezo mmoja tu kwa mwaka huu wa 2016 kutokana na muda mwingi kuuguza majeraha yake, kimsingi ilikuwa vigumu sana kwa mchezaji huyo kuitwa timu ya taifa. “Amekuwa nje kwa miezi mitano, amefanya juhudi kubwa kurudi katika hali yake ya kawaida, lakini bado hatuwezi kumwani kwa asilimia kubwa”, alisema kocha wa Hispania Vicente del Bosque.
Kiungo: Kevin Mirallas (Ubelgiji)
Kiungo huyu amekosa kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa kutokana na kutokuwa na msimu mzuri kunako klabu yake ya Everton, ambapo amecheza michezo 30 tu katika michuano yote msimu huu na kufunga magoli sita. Kukosa kwake nafasi kubwa ya kucheza katika klabu ndiyo sababu kubwa ya kuachwa kwenye kikosi cha Ubelgiji.
Mshambuliaji: Danny Welbeck (England)
Danny Welbeck alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Manchester City.
Awali Welbeck alikuwa na nafasi kubwa ya kuitwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa mpaka pale alipopata majeraha kwenye mchezo katika timu yake ya Arsenal na Manchester City ambao uliisha kwa sare ya 2-2. Majeraha hayo ya goti yatamfanya kuwa nje kwa takriban miezi nane.
Mshambuliaji: Diego Costa (Hispania)
Costa ametemwa kwenye kikosi cha Hispania kutokana na kutokuwa na msimu mzuri katika klabu yake ya Chelsea. Pia alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Liverpool mwezi ulioisha kwa sare ya bao 1-1. Hivyo kocha amekuwa na mashaka na utimamu wake kama angeweza kujitoa kwa asilimia mia moja.
Mshambuliaji: Mario Balotelli (Italy)
Mario Balotelli amekuwa katika kiwango kibovu kabisa katika maisha yake ya soka.
Akiwa amefunga goli moja tu kwenye EPL akiwa na Liverpool kabla ya kutolewa kwa mkopo kuelekea AC Milan, Balotelli amekosa nafasi ya kuitwa timu ya taifa ya Italy. Beki wa Italy Leonardo Bonucci anadhani kwamba mtazamao wa Balotelli ndiyo umemgharimu. “Angekuwa mtu muhimu sana katika timu yetu, lakini hakuna muda tena wa kubembelezana, tunapswa kuwa watu wenye kujitolea kwa moyo wote kwa ajili ya timu na wachezaji wenzetu” alisema Bonucci.
Kwenye benchi.
Jack Butland alipata majeraha wakati wa mchezo wa kirafiki kati ya England na Ujerumani mwezi March ulioisha kwa England kupata ushindi wa mabao 3-2.
Jack Butland (Stoke na England), Gokhan Inler (Leicester na Uswizi), Jesus Navas (Man City and Hispania), Gael Clichy (Man City na Ufaransa), Fabio Borini (Sunderland na Italy), Nacho Monreal (Arsenal na Ufaransa) Alen Halilovic (Barcelona na Croatia).