SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 29 Mei 2016

T media news

Serikali yatangaza kuisafisha Sekta ya Elimu na Watumishi wa umma wenye vyeti bandia.

Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa kampeni ya kuwashughulikia na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi wote walioajiriwa katika  sekta hiyo  wakitumia vyeti bandia .

Aidha, imewataka watumishi hao waanze kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe kabla ya kufikiwa na mabadiliko makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na utumishi wa umma yanayokuja nchini.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi Prof.Joyce Ndalichako wakati wa majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Amesema Serikali ya awamu ya tano imejipanga kufanya mabadiliko makubwa katika Sekta ya Elimu nchini ili kuhakikisha kuwa Elimu inayotolewa katika shule, vyuo na taasisi mbalimbali inazalisha wahitimu wenye sifa na ubora kwa maslahi ya Taifa .

Amesema katika kulitimiza hilo Serikali itawachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria watendaji wote walioshiriki na wale wanaoendelea kushiriki kwa namna moja au nyingine kukwamisha maendeleo ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na wale waliohusika katika udahili wa wanafunzi wasio na sifa katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Songea.

"Serikali ya awamu ya tano imedhamilia kwa dhati kabisa kuboresha kiwango cha elimu yetu kwa kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu, naomba niwahakikishie kwamba pale panapohitajika kufanyika mabadiliko tutayafanya bila woga" Amesisitiza.

Amesema katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za elimu hapa nchini, serikali imejipanga kubadilisha mfumo wa elimu ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu na kwamba mabadiliko hayo yatafanyika kwa kuwashirikisha wadau wote wa sekta hiyo.

" Tunapotaka kufanya mabadiliko kwenye mfumo wetu wa elimu tumekubali kwamba tuna changamoto,  katika changamoto hizi lazima tuwe na mahali pa kuanzia hivyo tunapochukua hatua tunaomba Watanzania mtuunge mkono"Amesisitiza Prof.Ndalichako.

Prof.Ndalichako Amesema lengo la Serikali kupitia Wizara yake ni kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa hapa nchini kwa kuendelea kutoa wahitimu bora wanaokidhi vigezo na viwango katika soko la ajira.

Amesisitiza kuwa mkakati wa Serikali ni kuanza kuwafuatilia wahitimu wote wasio na viwango ambao wako katika maeneo mbalimbali ya ajira huku akisisitiza kwamba elimu ya Tanzania ni sawa na kiwanda kinahitaji malighafi nzuri ili kitoe bidhaa bora.

Ameeleza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuvikagua vyuo vyote vinavyotoa elimu ya juu kuona kama vinakidhi sifa na vigezo vya kiutendaji ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale wote wanaowadanganya wananchi  na kuwapotezea muda vijana wanaowadahili bila kuzingatia sifa.

"Wizara yangu tunaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tuchukue hatua kwa wote walioichezea sekta hii muhimu, tulichofanya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph kinaendelea kwa vyuo vingine"

Kuhusu ujenzi wa maabara amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 12 kwa ajili ya kununulia vifaa vya maabara kwa shule zote 1536 ambazo zimekamilisha ujenzi wa majengo ya maabara kote nchini.

Katika hatua nyingine amesema kuwa Serikali katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 itafanya ukaguzi wa vyuo vyote vya Maendeleo ya Jamii kote nchini ili majengo ya vyuo hivyo yaweze  kutumika kuanzishia vyuo vya Ufundi Stadi VETA katika wilaya na mikoa ili kuwapatia stadi za kazi vijana waweze kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe.

Kwa upande wao baadhi ya Wabunge waliopata nafasi ya kuchangia wakati wa Kupitisha Bajeti ya wizara hiyo wameiomba Serikali kuweka mkazo katika usimamizi wa Sekta ya Elimu nchini ili shule, Taasisi na vyuo vya Tanzania vitoe wahitimu wenye ubora kwa maslahi ya Taifa.

Aidha, wameiomba Serikali kupitia Bajeti hiyo itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi wa shule, kuboresha maslahi na kulipa madai ya walimu pamoja na kuziimarisha Mamlaka za Udhibiti wa Elimu ili ziweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.