Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli leo ameweka Jiwe la msingi katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela zilizopo jijini Dar es Salaam ili kuanza kwa ujenzi wa barabara za juu (Fly Overs) zitakazosaidia kupunguza foleni.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Rais Magufuli amewataka viongozi wa jiji la Dar es Salaam kuhakikisha jiji linakuwa safi na lenye mandhari ya kuvutia ili kulinda afya za wakazi waishio humo.
Mbali na hayo pia amewaonya viongozi wa Jiji hilo kutoweka makampuni yao binafsi ya kufanya usafi ili kuepusha mgongano wa kimaslahi.
Akasema ” Viongozi wa Dar es Salaam msiweke Makampuni yenu yawe ndio yanafanya usafi, mkiyaweka mnategemea nini?” alihoji Rais Dk. Magufuli.
Mwakilishi wa JIKA nchini, Tishio Nagase amesema ujenzi huo wa mradi wa ‘Flyover’ uliopo chini ya ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Japan utaboresha maisha ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam kwa kupunguza foleni kwa kiasi kikubwa.
Nagase amewahakikishia Watanzania hadi kufikia Oktoba 2018 mradi huo utakuwa umekamilika kwa kiasi kikubwa.
Aidha Serikali ya Japan kupitia kwa Balozi wake hapa nchini, Masaharu Yoshinda amesema anafurahishwa kuona miundombinu inayojengwa na Japan ikizidi kutumika kwani uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Japan unalenga kuinua maisha ya wananchi
