SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 26 Machi 2016

T media news

Maoni: Hofu yangu Kuhusu Label ya Wasafi, Diamond, Harmonize na Raymond ni Kama ‘Mtu Mmoja’


Makala imeandikwa na Wynjones Kinye (Mhadhiri chuo kikuu cha SAUT)

Naappreciate sana juhudi za Diamond katika kuunyanyua muziki wa Tanzania kwa kuibua vipaji vipya kama Harmonize, Raymond na watakaofuata kama wapo.

Ni dhahiri kuwa kwa hili la kusimamia vijana wawili tu kiasi kikubwa cha fedha kimetumika na kinaendelea kutumika hasa ukizingatia kuwa Diamond tayari ni mtu sensitive kwenye quality ya product, na tunajua kuwa quality ni gharama kubwa siku hizi kama sio siku zote.

Diamond amethubutu kuwekeza, kibiashara tunategemea return katika kila unachofanya ‘kibiashara’ hivyo ni muhimu sana kufikiria vitu vingi vya kuifanikisha biashara ukiachana na mtaji. Hata kama una mtaji mkubwa na fedha za ziada kuuendeleza mradi bado failure iko pale kama hutotazama vitu vingine kwa kina.

Licha ya nguvu nyingi anayoweka Diamond kwenye muziki wa vijana wake ‘publicity na video nzuri’ bado mimi nina hofu ya kufanikiwa kwake kuwafikisha vijana wake hawa chini ya label yake. Nilivumilia kulisema hili baada ya kumsikiliza Harmonize, ila sasa nimeshindwa kukaa nalo baada ya kumsikia Raymond.

Naadmit kuwa hawa vijana Raymond na Harmonize wana vipaji vikubwa, wana sauti nzuri sana na ni waandishi vizuri lakini wanakosa kitu cha kuwafanya kuwa brand. Yupo mwandishi mmoja anaitwa Angela Cross alisema…

“Your brand is the foundation of your relationship with your audience – so be mindful of who your audience is (and no, it’s not “everyone”), what they want, and how you can connect with and serve them.”

Najua brand ni neno pana na kila mtu anaweza kulitetea kivyake kutokana na mapenzi na uelewa kwenye suala husika, vyovyote iwavyo niseme Diamond, Raymond, na Harmonize ni “MTU MMOJA.” Yaani ukitoa sauti zao (ambazo pia sasa zinaelekea kufanana) vingine vyote ninafanana zaidi.

Hapa nazungumzia uandishi wao, mawazo yao katika nyimbo, mtindo wa nyimbo zao, uandishi wao, na strategies za kibiashara ambazo naweza sema ni zile zile ambazo ameziexperience Diamond. Sasa kwanini tusifikirie brand kama ‘MUHURI’ ambao utakutambulisha kwa audience kama zilivyo documents zenye huo muhuri maofisini?

Haya, dalili zinaonyesha kuwa Richard Mavoko ataingia kwenye Label ya Wasafi. Ikitokea basi ni kheri lakini ni wazi pia kuwa kutaongeza ‘mlundiko’ wa mfanano katika muziki kwani hata mtu asiyefuatilia sana anafahamu kuwa Richard kwa matoleo kadhaa amekuwa akifanana sana kiuimbaji na Diamond, hata uachiaji wa nyimbo zao ulikuwa ukifuatana. Mbona yanaweza kuepukika haya? Tazama Harmonize anavyojaribu kuwa na attitude ya kwako.

Najua Diamond uko karibu sana na vijana wako, naamini wako huru kuzungumza nawe, uhuru huu sasa naona usifike kwenye muziki unaofanya, naona vitu viwili hapa na sina uhakika kipi ni kipi, kwamba vijana ni mashabiki wa muziki wako hivyo wanajikuta wanafanya unachofanya ama wewe ni bosi wa vijana na unawaambia nini cha kufanya ili ikurahisishie wewe kuwafanikishia ndoto zao.

Sijawahi kumsikia Raymond kabla, nilipata shauku kubwa kumsikia baada ya kujua kuwa yuko chini ya Wasafi, lakini shauku kubwa zaidi niliipata baada ya kusikia kuwa ni mtumiaji wa guitar katika uimbaji. Nilipata mawazo kadhaa ya picha juu ya huyu jamaa atakavyokuwa anaimba, niliamini angekuwa tofauti na Harmonize, niliamini angekuja na nyimbo tofauti na tulizozizoea siku hizi na niseme tu kuwa nilikuwa so disappointed.

Wimbi hili halipo kwa Wasafi tu,. naona balaa hili kutokea kwa Mkubwa na Wanawe. Angalia uimbaji wa Yamoto Band na wale wadogo zao, balaa linaendelea baada ya kumsikia mshindi wa BSS ‘Kayumba’ ambaye pia ni zao la Fella na sasa yupo chini ya usimamizi unaomhusisha Fella na washirika wake. Kayumba naye kaja na muziki uleule unaofanywa na wenzake wanaomzunguka.

Diamond!! Kama umeamua kusimamia wasanii nakushauri kuwaza ‘utofauti’, utofauti na upya ni must katika soko la muziki duniani kote especially sasa hivi, ni dhambi kubwa kibiashara kuwa ‘COMMON.’ Uimbaji na uandishi vya wasanii wako hakikisha vinatofautiana na vya kwako. Kama umemudu kuajiri mwalimu wa ‘kizungu’ kwa ajili ya crew yako basi hautoshindwa kuajiri mtaalamu wa kuwatengeneza tofauti vijana wako kwa kila kitu, hii kazi usiifanye wewe tafadhali.

Kwanini usitushangaze kwa kuja na vijana wenye muziki wa kitofauti na uufanyao wewe? Kuna ugumu gani kututengenezea kichwa kingine cha RnB kikatoa changamoto kwa wakina Ben Pol na Jux?

Kwanini usiufikirie muziki wa Grace Matata na Damian Soul pia? Vipi kuhusu muziki mzuri uliofanywa na Mandojo na Domokaya na kushindwa kuvuka mipaka? Huoni kuwa hivi vinavyotokea vinafanya tuchoke muziki (kitu ambacho ni makosa makubwa), hatupaswi kuuchoka muziki, fanyeni tusiuchoke muziki.

Nia yako ni nzuri sana Diamond na uzuri ni kuwa unaimudu kabisa nia hiyo (kitu ambacho ni muhimu sana), lakini kwanini sasa ugharamike isivyostahiki kwa kutumia nguvu tele kisa tu hujaweka mawazo yako/yenu nje ya vitu visivyohusisha fedha? Hofu yangu iko hapo zaidi, matumizi makubwa ya pesa isivyostahiki.