Jumuiya ya Madola (Commonwealth) imeipokea na kukubali dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kumpokea na kuwezesha ziara ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu, Dkt. Lazarus Chakwera, na msafara wake.
Ziara hiyo inalenga kuchunguza masuala ya uminywaji wa kidemokrasia na ukosefu wa utawala wa kisheria kufuatia matukio ya kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya kikao cha 72 cha Kamati Maalum ya Jumuiya ya Madola (CMAG), inayoshughulikia masuala ya demokrasia, utawala bora na haki za binadamu. Katika kikao hicho, Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), alikutana na kamati hiyo kujadili mazungumzo ya pamoja.
Tanzania ilibainishwa katika ajenda maalum ya CMAG baada ya kikao chake cha 71 Disemba 2025 kilichoongozwa na Dkt. Ian Borg, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Utalii wa Malta. Katika kikao hicho, Tanzania ilitakiwa kuhakikisha msafara wa Katibu Mkuu unapata nafasi kamili bila vizuizi kukutana na wadau wote, kuondolewa kwa vizuizi vya uhuru wa kukusanyika na kujieleza pamoja na upatikanaji wa vyombo vya habari, kufanyika kwa majukwaa ya mashauriano kati ya vyama vya siasa kuelekea uchaguzi ujao, na kuchukua hatua za kisheria na kiutawala dhidi ya wahusika wa vurugu pamoja na kutoa fidia kwa waathirika pale inapofaa.
Ujumbe huo unaotarajiwa kuongozwa na Rais mstaafu wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera, unatarajiwa kufika Tanzania mwezi Machi 2026 huku miongoni mwa taarifa za rejea zinazotumika ni ripoti ya Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uchaguzi, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi.
