SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 8 Mei 2018

T media news

Kampuni ya Maxmalipo yatangaza kupunguza wafanyakazi

Kutokana na mabadiliko ya teknolojia kampuni ya Maxcom Africa imetangaza kuajiri wafanyakazi wapya wenye ujuzi unaohitajika.
Kutokana mabadiliko hayo, baadhi ya wafanyakazi waliopo ambao ama nafasi zao zitakufa kutokana na teknolojia mpya inayotumiwa na kampuni hiyo au zitakuwa zinajirudia hivyo kuilazimu kuwapunguza.
Msemaji wa Maxcom Africa, Deogratius Lazari  amesema  kwa sasa kampuni hiyo ina watumishi 451 lakini baada ya Serikali kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki kwenye masuala mengi mfano utoaji wa zabuni, ukusanyaji wa mapato na maeneo mengine, baadhi ya majukumu yamepungua huku mengine yakizaliwa.
“Huwezi kurundika wafanyakazi wengi kwenye eneo moja bila kujali tija yao. Tulipunguza baadhi ya wafanyakazi walioonekana ufanisi wao upo chini mwaka jana ila awamu hii ni kutokana na mabadiliko ya teknolojia,” amesema Lazari.
Amesema yapo maeneo kadhaa ya operesheni za kampuni hiyo ambayo yameimarishwa kiteknolojia kurahisisha majukumu ya menejimenti, wafanyakazi na mawakala zaidi ya 15,000 waliopo nchini kote.
Taarifa ya uwezekano wa kupunguza wafanyakazi wake iliyotolewa na mkurugenzi wa uendeshaji wa kampuni hiyo, Charles Natai inasema utaratibu wa kisheria utazingatiwa kufanikisha mchakato huo kwa wafanyakazi watakaolazimika kupunguzwa. Taarifa ilitolewa Mei 4.
“Jambo hili linatufanya sisi kufanya uamuzi wa kupitia upya mfumo wa uendeshaji wetu na kuboresha miundombinu ya shirika ili kufikia mahitaji yetu ya kibiashara wakati tukiimarisha ufanisi,”  inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.