Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dk Reginald Mengi ameingia ubia na Mwekezaji kutoka India kujenga kiwanda cha dawa kitakachogharimu dola za kimarekani milioni 55 sawa na shilingi bilioni 55 za Tanzania.
Ujenzi wa kiwanda hicho kipya kiitwacho M- pharmaceutical Ltd, katika eneo la Kerege, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani umewekewa jiwe la msingi na Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu mwishoni mwa wiki.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alimpongeza Dr Mengi kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais John Magufuli alilolitoa wakati wa uzinduzi wa hospitali mpya kisasa ya Taaluma na Tiba Muhimbili Mlonganzila.
Novemba mwaka jana akifungua Hospitali hiyo katika hotuba yake Rais John Magufuli aliwataka wafanyabiashara nchini kuanzisha viwanda vya dawa kwa kuwa fedha nyingi zinatumika kuagiza dawa kutoka nje.
Dk Mengi ambaye pia ni Rais wa sekta binafsi alikuwepo katika uzinduzi huo na kusema kwamba yeye na wenzake watalitafakari rasmi suala hilo.
Waziri Ummy Mwalimu pia amemhimiza Dr Mengi na mbia mwenzake kuharakisha ujenzi wake na kumhakikishia kuwa bidhaa zitakazozalishwa zitapata soko kubwa hapa nchini na nchi za ukanda huu, na kunufaika na upendeleo maalum wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dr Reginald Mengi amesema katika awamu ya kwanza kiwanda hicho kitazalisha chupa milioni 30 kwa mwaka za aina mbalimbali za maji ya dripu zinazotumiwa wakati wa matibabu ya dharura nyakati za ajali, upasuaji, homa kali, na magonjwa ya mlipuko, zinazokidhi vigezo vya kimataifa.
Amesema kipaumbele cha ajira kitatolewa kwa wananchi wa Bagamoyo, na kusisitiza kuwa umuhimu wa Watanzania kujiamini katika kujiletea maendeleo.
Mapema Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Dk Charles Mwijage na Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikiro amewataka viongozi wasiwakwamishe wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika maeneo yao.
Aidha walisema kwamba serikali itashughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maji, umeme wa uhakika na gesi asilia katika eneo hilo.
Alisema kwamba taifa linajenga uchumi wa viwanda na ni kazi ya serikali kuwezesha mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji.
Uwekaji jiwe la msingi ulishuhudiwa na wananchi wa Kerege, Balozi wa Ufaransa Frederic Clavier, balozi wa China Wang Ke, Mbunge wa Bagamoyo Dr Shukuru Kawambwa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno na viongozi mbalimbali mbalimbali wa serikali na CCM wa mkoa na wilaya ya Bagamoyo.