Baadhi ya wanaume wa Mkoa wa Dar es Salaam leo wamejitokeza kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, baada ya kusikia tangazo kutoka kwa mkuu huyo juu ya kufika ofisini kwake kwa malalamiko ya kutelekezewa watoto na wanawake.
Wanaume hao walikuwa gumzo kwa watu wengi kwa ujasiri huo wa kufika kwa mkuu wa mkoa ili kudai haki zao baada ya kutelekezwa na wake zao.
Mmoja wa wahanga hao aliyejitambulisha kwa jina la Tito Petro alishtua wengi baada ya kutoa kauli kuwa ugonjwa wa kupooza ndiyo chanzo kikubwa cha kusambaratika kwa familia yake.
Agizo hilo la wanaume kujitokeza leo, alilitoa Makonda jana baada ya siku ya kwanza ya kuanza kusikiliza kero mbalimbali za wanawake wa mkoa wake waliojitokeza kwa ajili ya kuelezea kero zao juu ya kutelekezewa watoto ili wapate msaada wa kisheria kutoka kwa maofisa ustawi wa jamii, Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia na Ofisi ya Mkemia mkuu wa serikali.
Wanaume waliofika ofisini hapo awali walikuwa wakiogopa kuingia ndani lakini baada ya kusikia tangazo lililokuwa likitolewa na mkaribishaji wa wageni wa eneo hilo, walianza kuingia ndani mmoja baada ya mwingine.
Akizungumza jana na akina mama waliofika kwa ajili ya malalamiko, Makonda alisema zoezi hilo litaendeshwa kwa muda wa siku tano ili kuhakikisha kila mwanamke anayefika ofisini kwake anasikilizwa kwa umakini na mwisho wa siku atendewe haki pasipo kuvunja sheria.
Aidha Makonda alisema atahakikisha mwanamume yeyote aliyemzalisha mwanamke na kumtelekeza anatafutwa popote alipo ili aweze kutoa matunzo ya mtoto na mwisho wa siku mtoto afurahie fursa ya elimu bure.