Mkurugenzi Msaidizi wa Kampuni ya Lake Oil, Halid Mohamed na Mkurugenzi wa Miradi wa kampuni hiyo, Fahim Mohamed wamekamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kukiuka sheria za uwekezaji katika ufukwe wa Bahari ya Hindi Wilaya ya Kigamboni.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es salaam, Hashim Mgandilwa aliagiza kuwekwa chini ya ulinzi maafisa hao wawili wa juu wa kampuni ya mafuta ya lake oil kwa kukiuka masharti ya uwekezaji katika eneo la fukwe za bahari.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kigamboni imechukua hatua hiyo baada ya kampuni ya Lake Oil kukaidi amri ya kutakiwa kubomoa gati pamoja na majengo yanayosadikiwa kutumika kupokea na kuhifadhi mali za magendo.