SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 4 Aprili 2018

T media news

Vodacom yasitisha huduma ya kuuza LUKU

Kutokana na kutokidhi masharti ya mfumo wa malipo serikalini (GePG), Vodacom imesitisha huduma za malipo ya Luku kwa wateja wake wa M-Pesa.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa Vodacom, Rosalynn Mworia amesema wanaendelea na mazungumzo na Serikali kupata muafaka kabla ya
kurejesha huduma hiyo.

“Huduma ya Luku imesitishwa mpaka makubaliano na Serikali yatakapokamilika. Tunachukua juhudi za makusudi kuhakikisha muafaka unapatikana na huduma kurejea kama kawaida,” alisema Mworia.

Mfumo mpya wa ununuzi wa Luku ulianza kutumika Aprili 2 na wateja wanaotumia huduma za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wanatakiwa kuufuata ili kuendelea kupata huduma.

Meneja wa Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji alisema jana kwamba baada ya kuanza kutumika kwa mfumo huo, uhusiano kati ya shirika
hilo na wauzaji wengine wa umeme umekoma.

Alisema kuanzia sasa, mkataba wa kuuza nishati hiyo unafanywa baina ya wakala na Serikali.

“Zamani mawakala wote walikuwa wanapitia Tanesco lakini sasa wanatakiwa kujiunga na mfumo wa Serikali. Baadhi wamekamilisha
utaratibu wengine wanaendelea kukamilisha,” alisema Leila.

Hata hivyo, alisema wateja wanaotumia mita za Luku wataendelea kupata huduma kutoka ofisi za shirika hilo, maduka ya Tanesco na vituo vya mafuta, mawakala wa Selcom na Maxcom na benki za CRDB na NMB.

Kwa wateja wanaotumia simu za mkononi, Kampuni za Tigo, TTCL na Airtel ndizo zilizokamilisha masharti ya kuweza kuendelea kutoa huduma hiyo.

Licha ya Vodacom, Leila aliitaja mitandao mingine ambayo ipo kwenye hatua za kujiunga kwenye mfumo huo kuwa ni Halotel na Zantel.

“Maboresho yanaendelea kutatua changamoto kadhaa zilizojitokeza. Tutaendelea kuwajulisha namna bora ya kupata huduma za Luku,”
alisema Leila.

Meneja mawasiliano wa Halotel, Mhina Semwenda alisema majadiliano na Serikali yamekamilika na kuanzia leo watakuwa wameunganishwa kwenye mfumo mpya.

“Kuanzia saa sita usiku leo (jana) Halopesa watakuwa wanajiunga kwenye mfumo wa Serikali. Majaribio yatafanywa muda huo kwa sababu kunakuwa na wateja wachache na baada ya hapo huduma itaendelea kutolewa kama kawaida,” alisema Semwenda.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyoletwa na mfumo mpya ni kupungua kwa kamisheni iliyokuwa inalipwa kwa mawakala wanaohudumia
wateja mtaani.

Hata hivyo, taarifa ambazo hazikuthibitishwa zinadai kwamba asilimia za malipo kwa mawakala zitapungua chini ya mfumo huo mpya.

Mkuu wa kitengo cha masoko na ubunifu wa kampuni ya Maxmalipo, Deogratius Mosha alikiri kuwapo kwa mabadiliko ya malipo bila
kubainisha kiasi akisisitiza kuwa taarifa hizo ni siri baina yao na mawakala na si jambo la kuweka wazi kwa vyombo vya habari.

“Ninachoweza kusema ni kuwa huduma zetu zinaendelea kama kawaida licha ya mabadiliko madogo yaliyojitokeza. Tayari tumeunganishwa kwenye mfumo wa Serikali. Siwezi kulisemea suala la malipo kwa kuwa kila wakala ana uhuru wa kuendelea na biashara au kujiondoa,” alisema Mosha.

Mmoja wa mawakala wa Maximalipo jijini Dar es Salaam, Martha Joseph alisema alipata ujumbe kutoka Maximalipo kuwa kutakuwa na
mabadiliko ya kimfumo kuanzia Aprili 2 lakini huduma zitaendelea kama kawaida na malipo yake hayatabadilika.

Kutokana na ujumbe huo, alisema aliwasiliana na ofisa anayemhudumia kupata ufafanuzi zaidi ambaye alimhakikishia kuwa huduma
zitaendelea kama kawaida lakini kutakuwa na mabadiliko ya malipo yatakayopungua kidogo.

“Sijapata ujumbe maalum lakini huyo kaka aliniambia malipo yatapungua. Zilipoondolewa faini za polisi kutumika huduma za MaxMalipo, faida yalipungua, sijui hili nalo litakuwa na athari kiasi gani katika baishara,” alisema Martha.

Chanzo: MWANANCHI