Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo ameanza kusikiliza malalamiko kutoka kwa wanawake waliozalishwa kisha kutelekezwa na wanaume.
Shughuli hiyo ambayo itadumu kwa siku tano, inafanyika katika ofisi za mkuu huyo wa mkoa, Ilala Boma, huku idadi kubwa ya wanawake na watoto ikijitokeza.
Taarifa za kuaminika zinaeleza kuwa kutokana na utaratibu huo, hofu imetanda kwa baadhi ya viongozi wa serikali, dini, wanasiasa na maofisa waliowapa mimba kisha kuwatelekeza wanawake.
Pia, imedaiwa kuwa hali ni mbaya kwa wanaume viwembe, hususani waliochepuka nje ya ndoa zao, ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa hawataki kujulikana kama wamezaa nje ya ndoa ili kuficha fedheha.
Wengine ambao mambo yao yatawekwa hadharani ni vigogo waliowazalisha wasaidizi wa kazi za ndani pamoja na wafanyakazi wao maofisini.
Akizungumza wakati wa kutangaza operesheni hiyo, makonda alisema amebaini baadhi ya viongozi serikalini, wabunge, vionozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa, wanahusika kwa kiasi kikubwa kuwazalisha wanawake na kuwatelekeza.
“Wengi waliowapa mimba wanawake ni watu wenye ndoa, hivyo hawataki watoto au wanawake hao wajulikane ili kulinda ndoa zao. Vigezo vyao ni kutomtambua mtoto wa nje,” alisema.
Aliisema katika kuficha haki ya watoto, baadhi ya viongozi wameamua kuanzisha vituo vya watoto yatima ambapo ndani ya vituo hivyo huwahifadhi watoto waliozaliwa nje ya ndoa.
“Je, ni halali kwa mtoto mwenye baba na mama, tena wenye kipato cha kutosha kuhifadhiwa katika vituo vya yatima?” alihoji makonda.
Aliongeza “Tunao viongozi wengi wa serikali waliotelekeza kinamama na mtawashuhudia hapa.”
Alisema kwa mwanaume ambaye atakataa mtoto, ataingizwa kwenye gari na kupelekwa kwenye ofisi ya mkemia mkuu kwa ajili ya kupimwa vinasaba (DNA).
“Hadi tumjue mtoto ni wa nani, hivyo na nyie kinamama muwe wakweli, siyo kusingizia wanaume. Ukija hapa uwe na uhakika na mwanaume husika,” alisema.
Foleni ya wanawake waliofika kuwasilisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda asubuhi leo.