I: Upendo/Mapenzi Ni Nini?
Watu wengi huuliza upendo au mapenzi ni nini? Kila mtu anaweza kuwa na majibu yake. Lakini kiuharisia mapenzi au upendo ni shauku ya mahusiano yenye nguvu na matumaini ya kujali nafsi au kitu fulani inayomea katika nafsi ya kiumbe hai! Hii ndio tafsiri ndogo lakini ya kina inayoweza kuelezea nini maana ya mapenzi.
II: Aina Za Upendo
Kuna aina tatu kubwa za upendo zinazofahamika. Aina hizo ni Upendo wa Agape, Upendo wa Kimaumbile na Upendo wa Kimahaba.
A: Upendo wa Agape
Aina hii ya upendo inaaminika anao MUNGU pekee kwa kuwapenda viumbe wake. Msingi mkubwa wa aina hii ya upendo ni imani. Leo hii sitauzungumzia upendo wa aina hii!
B: Upendo wa Kimaumbile
Upendo wa kimaumbile ni aina ya upendo unaotokana na kuhusiana kwa chembechembe za kimaumbile baina ya wapendanao. Kwa lugha nyingine huu ni upendo wa ndugu wa damu kwa mfano kaka na dada, baba na mtoto, mama na mtoto nakadhalika. Msingi mkubwa wa aina hii ya upendo ni udugu wa damu!
C: Upendo wa Kimahaba
Aina hii ya upendo ndio nitakayoizungumzia kwa leo. Upendo wa kimahaba ni shauku yenye nguvu na matumaini ya kujali inayoambatana na msukumo wa hisia za ngono! Aidha msingi mkubwa wa aina hii ya upendo ni ngono na hakuna upendo wa kimahaba usiohusisha ngono!
III: Aina Za Upendo Wa Kimahaba
Kuna aina tatu za upendo wa kimahaba. Aina hizi zimegawanywa kulingana na mfumo au muundo wake. Aina hizi ni:
A: Upendo Sumaku
Aina hii ya upendo ni nadra sana kutokea japo huwa unatokea. Upendo sumaku hutokea wakati nafsi mbili zinapendana na kuridhiana kwa kila hali mara ya kwanza tu baada ya kuonana! Ni kweli aina hii ni nadra sana kutokea yaani unakutana na mtu kwa mara ya kwanza mnapendana kwa dhati na hamwoni kasoro machoni kwenu wala mioyo yenu haishuhudii majuto ya kupendana kwenu!
Faida Zake
1. Jitihada na nyenzo kidogo sana hutumika kuimarisha aina hii ya upendo kwa sababu ni upendo unaoota katika nafsi zote mbili kwa panoja.
2. Ni upendo rahisi kwa sababu wahusika hujifunza na kuzoea haraka sana tofauti zinazojitokeza baina yao.
3. Hukua kwa haraka zaidi.
4. Una furaha ya kweli.
Hasara Zake
1. Ni nadra sana kutokea.
2. Unaweza ukadumu au usidumu, hautabiriki.
3. Una mambo mengi ya kushtukiza kutokana na ukweli kwamba wahusika hufika mbali wakati hawajajuana vema!
4. Mwisho wake huwa hautabiriki.
B: Upendo Upande Mmoja
Aina hii ya upendo hujitokeza katika nafsi moja na nafsi nyingine hufundishwa kupenda baada ya muda fulani kupita. Hii inatokea nafsi moja inapenda nafsi nyingine ambayo haikuwa hata na mawazo ya kuwa katika mapenzi na hiyo nafsi mwenza. Aina hii ya mapenzi imetawala sana duniani, yaani mmoja anaanza kupenda ndipo anamfundisha mwenzake pia kumpenda.
Faida Zake
1. Ni upendo imara na madhubuti.
2. Wahusika wana nafasi ya kujuana kiundani.
3. Mara nyingi unadumu sana.
4. Mwisho wake hufahamika, yaani ni uhusiano unaofahamika kama utadumu au hautadumu, utaisha au hautaisha.
Hasara Zake
1. Hutumia rasilimali nyingi na nguvu nyingi kuujenga.
2. Huchukua muda mrefu kujengeka.
C: Upendo Mazoea
Kama lilivyo jina lake, aina hii ya upendo hujengeka kutokana na mazoea ya kimazinngira mfano kazi, makazi au kuchangia aina fulani ya shughuli inayokutanisha wahusika wawili kwa muda mrefu. Kwa mfano mke na mume wakiwa ni wafanyakazi katika ofisi tofauti, kinachotokea ni kwamba wanapokuwa makazini wanatumia muda mrefu sana kuzoeana na watu ambao wanawazunguka katika mazingira yao ya kazi. Mke anaweza akazoeana na mwanaume mwingine kazini kwa sababu zaidi ya saa nane akiwa na nguvu anakuwa na huyo mtu siku zote za maisha yake. Kwa muda usio zidi saa tatu anakuwa na mume wake wakiwa macho na baada ya hapo wanalala kila mtu anakuwa hayuko na mwenzie katika ufahamu wote.
Ndio maana ni rahisi sana kwa mwanamke kama ni msaidizi wa bosi wake kuwa na mahusiano naye kwa sababu ya mazoea. Hii hutokea na kwa upande wa wanaume pia. Umewahi kusikia au kuona watu wanakutana kwa mara ya kwanza na hawapendani kabisa na kila mmoja anakuwa anaona ugumu kuwa na mwenzake lakini inawezekana kazi ikawafanya wawe pamoja mara nyingi na kujikuta wanaanguka katika upendo pasipo kutambua? Kama umewahi kushuhudia basi hii ndio aina ya upendo mazoea.
Faida zake
1. Hauhusishi kumbukumbu za nyuma za wahusika.
2. Wahusika wanaweza kuudhibiti vizuri ili usiwaumize wengine, mfano mke na mume kuwa na mahusiano na wapenzi wengine.
3. Ukikomaa una hisia kali.
4. Hudumu sana.
5. Mara nyingi hutokea kwa kujifurahisha na kukidhi haja za kingono na matamanio.
Hasara Zake
1. Ni upendo wa hatari kwa sababu unaweza kuumiza hisia za wengine iwapo utafahamika.
2. Hauna matarajio na mipango ya baadae.
3. Mara nyingi uhusisha wahusika ambao wapo kwenye mahusiano mengine tayari na ya kudumu.
4. Mwisho wake hautabiriki na mara zote huwa unakuwa ni mbaya.