SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 7 Aprili 2018

T media news

Serikali yataja sababu ya kuzuia wenye miaka 25 kujiunga kidato cha 5

Kufuatia uamuzi wa kuweka ukomo wa umri wa miaka 25 kwa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya kidato cha tano katika shule za sekondari, Wizara ya Elimu imesema imechukua uamuzi huo licha ya kuwa, inatambua kwamba kila mwananchi ana haki ya kupata elimu.

Wizara imeeleza kwamba, imeweka ukomo huo kutokana na kwamba, kuchanganya wanafunzi wenye umri mkubwa na wale wenye umri mdogo kunaathiri mazingira yao ya kusomea.

“Pamoja na kwamba tunasema kuwa ni haki ya kila Mtanzania kupata elimu, na tunasema kwamba elimu haina mwisho. Lakini vile vile tunaangalia mazingira ua ujifunzaji ya wanafunzi wetu,” alisema Naibu Waziri wa Elimu William Ole Nasha.

Naibu Waziri amesema kuwa, kwa wanafunzi ambao tayari wamefikisha umri wa miaka 25, haimaanishi kwamba hawataweza tena kusoma, lakini akasema kuna njia nyingine wanazoweza kuzitumia kufika chuo. Alisema wanafunzi hao wanaweza kufanya mtihani wa kidato cha sita kama watahiniwa binafsi au wakajiunga na elimu ya watu wazima.

Aidha, Wizara imesema kuwa, kigezo hicho kimekuwapo siku zote na sio kipya. Pia, imeelezwa kwamba, kwa miaka yote ambapo wamekuwa wakitumia kigezo hicho hawakuwahi kupa waombaji wenye miaka 25, au 24 na badala yake wengi wanaoomba kujiunga na kidato cha 5 wana miaka 23 kushuka chini.