Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amekionya Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuacha kujishirikisha na masuala ya kisiasa na harakati, na iwapo watakiuka hilo, wasitarajie kupata ushirikiano wa aina yoyote kutoka katika Mahakama.
Prof. Juma amesema kwamba hawatawalazimisha TLS kuachana na masuala ya kisiasa, lakini wao watakachofanya endapo chombo hicho cha wanasheria kitakaidi agizo hilo, ni kutokutoa ushirikiano.
Ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano ya Azam Tv ikiwa ni siku chache tangu Rais Dkt Magufuli alipomtaka Jaji Mkuu kuhakikisha kuwa chama hicho ambacho ni mali ya umma hakiachwi kiendeshwe kama mali ya mtu binfasi.
Rais Dkt Magufuli aliyasema hayo Aprili 20 mwaka huu wakati akiwaapisha Majaji 10 wa Mahakama Kuu pamoja na viongozi wengine wa kisheria wa serikali, hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Tanganyika Law Society (TLS) ni sehemu ya mtiririko wa taaluma ya sheria inayoanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na vyuo vingine vinavyotoa degree ya sheria, Shule ya Sheria unayoingia mwanachama wa TLS na kuruhusiwa kufanya shughuli za kisheria,” alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu amesema kuwa, mtiririko huo unaonesha kuwa chombo hicho ni mali ya umma na sio mali binafsi. Katika kuendelea kutoa ufafanuzi kwa namna gani chombo hicho ni cha umma, alisema kwamba, mamlaka ambayo chombo hicho kimepewa, yanaonesha kuwa ni cha umma.
Moja ya majukumu yao ni kusaidia kuboresha elimu ya sheria na kuboresha taaluma ya sheria Tanzania, hivyo Jaji Mkuu akasema kuwa, jukumu hilo sio binafsi bali ni la umma.
Amekitaka chama hicho kuhakikisha kinabaki katika malengo ya msingi ya kuanzishwa kwake, na kwamba wakianza kujihusisha katika siasa baadhi ya watu ambao wanashirikiana nao hawata wapa ushirikiano kutokana na sheria kuwazuia kujihusisha na siasa.