Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Suzan Kolimba amesema Suala la Mauaji ya Kimbari sio jambo la kufikirika kwani limeshatokea katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu na ndio maana Serikali katika nchi hizo zimekuwa zikiandaa mikakati mbalimbali ili kuhakikisha tukio hilo linakuwa historia..
Dkt. Kolimba amesema hayo alipokuwa akifungua semina ya Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Katiba na Sheria na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambapo alimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi.
“Mauaji ya kimbari sio jambo la kufikirika, limeshawahi tokea katika nchi zetu, ndio maana kumekuwa na mikakati mbalimbali ili kuhakikisha mauaji kama hayo yanakuwa historia, tunataka mauaji haya yawe historia kwa nchi zetu na yasije jirudia tena,” alisema mhe. Kolimba
Alisema kwamba nchi za maziwa makuu kwa sasa zinatakiwa kuongelea maendeleo na mashirikiano na sio vita au ubaguzi wa aina yoyote ile.
Alisema viongozi wanatakiwa kujua kuwa wameshilikilia hatma za watanzania mikononi mwao na hivyo hawana budi kuweka mbele utu, uzalendo na utaifa dhidi ya tashwishi za kisiasa kwa mustakabali mzuri wa wananchi.
Mhe. Kolimba alitumia nafasi hiyo kuipongeza Tanzania na Kamati ya Kitaifa ya mauaji ya Kimbari kwa kuwa ni moja ya nchi zilizotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa zinafanya vizuri katika eneo hilo.
Kikao hicho kinachifanyika mjini Dodoma kinalenga kuwapitisha Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati hizo juu ya Mkataba wa Kuzuia mauaji ya kimbari kwa nchi za Maziwa Makuu wa mwaka 2006 ili kuwapatia uelewa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na ubaguzi dhidi ya binadamu.
Tanzania pamoja na nchi nyingine 12 za Maziwa Makuu walitia saini kuridhia utekelezaji wa mkataba huo. Nchi hizo ni pamoja na Kenya, Uganda,Rwanda,Burundi, Congo DRC, Sudani Kusini, Sudani,Zambia,Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Congo.
Semina hiyo ya wabunge imeandaliwa na Kamati ya Kitaifa ya kuzuia mauaji ya Kimbari nchini kwa kushirikiana na Ofisi ya Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia mauaji ya kimbari ya New York Marekani.