Je, leo unapofikiria maisha yako yaliyopita, unafurahi na kuridhika kuwa uliyaendesha vizuri au hauridhiki? Watu wengi husikitika hadi wakasema kama wengebahatika kupata nafasi kurudia maisha, wasingeishi kama walivyo sasa.
Wanasema wangekuwa makini zaidi katika kupanga maisha yao ili kuyafanya yawe bora zaidi.
Huenda hata wewe unafikiria hivyo. Lakini duniani tunaishi mara moja tu wala hatutarudi tena baada ya kufariki.
Hivyo nafasi tulitonaayo ndiyo hii ya kurekebisha maisha yetu. Na wala hatujachelewa.
Je tunawezaje kufanya maisha yetu yaliyosalia kuwa bora? Hebu tushirikiane kutaafakari kisa hiki tuone kama kitatusaidia kuboresha maisha:
Kijana aliyemaliza chuo kikuu alikwenda kwa mwanafalsafa kumuomba amsaidie kuamua kazi itakayomfaa zaidi. Yule mwanafalsafa akamuuliza “ Kwani wewe unataka kazi gani?” Kijana akajibu, “ Nimekuja kwako kwa sababu sijui cha kufanya”
Mwanafalsafa akamwambia Mimi sitaweza kukusaidia kama wewe mwenyewe hujui nini unachotaka.
Labda fikiri na uniambie baada ya miaka kumi kutoka leo unataka uwe umefikia hali gani ya maisha.
Kutaka ushauri kuhusu maendeleo yako katika maisha ni kama kwenda kukata tikiti ya usafiri. Wale wanao katisha tikiti hawataweza kukupatia tikiti mpaka uwambie lengo lako ni kwenda wapi.
Hivyo ukinipatia maelezo niliyokuomba nitaweza kukusaidia.
Yule kijana akasema “ Nataka baada ya muda huo niwe na maisha mazuri.
Niwe na kazi yenye mshahara mzuri, nyumba nzuri yenye fenicha ya kisasa,gari ndogo inayovutia na familia yenye maisha mazuri”
Kutokana na kisa hiki tumejifunza kuwa ni muhimu binadamu kuwa na malengo katika maisha. Lengo ni shabaha, nia, ama makusudi.
Hivyo kila wakati binadamu anapaswa kuwa na mambo anayofikiria kuyatekeleza ili kupiga hatua fulani anayotarajia katika katika maisha.
Kila siku tunawaona watu wakifanya shughuli mbalimbali.
Wakulima mashambani, wafugaji malishoni, wavuvi baharini na mitoni, warina asali na wapasuaji mbao misituni, wachimba madini migodini, mafundi viwandani, wafanya biashara madukani na masokoni na wajenzi kwenye majengo mapya. Aidha, kuna kundi kubwa la watumishi kama vile madaktari, wahandisi, wahasibu, mameneja, walimu, makarani, askari, walinzi na madereva na wahudumu mbalimbali.
Wote hawa ukiwauliza watakwambia wanashughulika ili kutafuta maisha.
Kwa hakika huwa wanatafuta kipato ili wakidhi mahitaji mbalimbali ya maisha kama vile chakula, malazi, mavazi na huduma kama vile elimu, afya, malezi ya watoto, burudani na huduma nyingine kadha wa kadha.
Pamoja na kushughulika kote huko bado kuna watu wenye maisha duni wakati wengine wana maisha bora.
Ajabu ni kuwa hata wale wanaofanya kazi ya aina moja na kupata mishahara inayofanana na wenye familia zilizo sawa, bado hutofautiana katika hali za maisha yao.
Kinachofanya watofautiane ni nini? Hakuna kingine chochote isipokuwa kuwa na malengo
Wakati mmoja niliwahi kujaribu kuwauliuza watu ninaokutana nao kama wana malengo ya maisha waliyoyaandaa.
Nilistaajabu kugundua watu wengi hawakuwa wameandaa malengo yoyote ya maisha na kulikuwa na wengine ambao hawakuelewa hata maana ya malengo na hawakutambua kama kuna haja ya kuandaa malengo.
Aidha, uchunguzi wangu ulionyesha kuwa watu waliofanikiwa katika maisha kuliko wengine ni wale ambao huhakikisha wakati wote wana malengo. Baada ya kuweka malengo Watu huwa hutumia akili na juhudi zao zote kuyatekeleza.
Baada ya kutambua kuwa kujiwekea malengo ndio ufunguo wa maisha bora sasa inabidi tujifunze namna ya kuweka malengo:
Jinsi ya kuweka malengo
Unapotaka kuweka malengo fuata hatua mbili zifuatazo
1. Kuweka taswira unayoitarajia baadaye
Kwanza fikiria katika akili yako uvute taswira unayoitarajia itokee au uifikie utakapo kamilisha lengo lako. Unapoweka taswira akilini fikiria sehemu tatu zinazo kuhusu yaani kazini, nyumbani na katika jamii
2. Kuchambua vigezo vya matarajio
Katika zoezi hili utataja vigezo vya mafanikio unavyotarajia kwa kujibu maswali kama vile, Ni kitu gani ninachotarajia kukifanikisha katika kipindi cha lengo? Je ninatarajia kuwa katika hali gani nitakapotimiza lengo? Kiwango gani cha mafanikio ninastahili kukifikia ili niridhishe nafsi yangu? Vigezo vichambuliwe kwa kujibu maswali kuhusu kazini, nyumbani na katika jamii. Ifuatayo ni mifano ya maswali.
Kuhusu kazini maswali yanaweza kuwa kama vile: Natarajia kufikia kiwango gani cha mshahara au mapato? Kuwa na madaraka au mamlaka kiasi gani? Kupata kiwango gani cha hadhi na heshima?
Kwa upande wa nyumbani maswali nikama vile: hali ya maisha ya familia yangu ipande juu kiasi gani? Watoto wangu wapate elimu ya kiwango gani? Nyumba ya kuishi iwe ya namna gani?
Kuhusu hali yangu katika jamii maswali yanaweza kuwa kama vile. Niwe na marafiki wa aina gani? Nijiunge na vikundi vya jamii vya aina gani? Nifanikiwe kupata madaraka au uongozi gani katika jamii?
Zoezi la kuweka malengo katika maisha litekelezwe kwa kufanya fikara zako ziwe huru kama vile mtu anayeota ndoto ya mambo yatakavyoweza kuwa baada ya miaka 5 au 10.
Daima hakikisha unaweka malengo na unafanya kila juhudi kuyatekeleza.