SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 14 Aprili 2018

T media news

Familia za ‘waliotekwa’ Zanzibar zatoa kauli nzito kwa serikali

Familia za vijana watatu wakazi wa Mtambwe Kisiwani Pemba waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa zaidi ya wiki moja sasa wamesema kuwa hawatakubali kupokea maiti katika mifuko endapo ndugu zao hao ambao hawajulikani walipo hadi sasa watakapopatikana wamefariki dunia.

Familia hizo zimetoa wito kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kuwa ndugu hao wanarejeshwa wakiwa hao kwani hawakuwa wahalifu wa tukio lolote lile.

Akizungumzia kuhusu kupotea kwa vijana hao, Masoud Juma Masoud ambaye ni Mzee wa Khamis Abdallah Mattar amesema kwamba yalifika magari mawili katika nyumba za wahanga hao majira ya saa 5 za usiku na kugonga kisha kuwachukua vijana hao.

Amesema kwa muda sasa wamekuwa wakifuatilia lakini hawajua ndugu walipo na kama wapo hai ama wamefariki. Pia alisema kwamba, Jeshi la Magereza lilisema kwamba vijana hao hawapo katika mahabusu yoyote visiwani humo.

Aidha, alieleza kwamba, licha ya kuwa waliokuja kuwachukua walisema ni maafisa magereza, lakini walipofuatilia waligundua kwamba magari ya usalama wa taifa ndio yaliyotumika, hivyo wanaitaka serikali kuhakikisha kwamba vijana hao wanarudi majumbani mwao salama.

Familia hizo zimeeleza mambo mengi ikiwamo namna wanavyopitia changamoto za kimaisha kutokana na ndugu zao waliotoweka ndio walikuwa tegemeo kubwa la kiuchumi, hivyo kwa sasa wamebaki pasi na msaada wowote, hivyo jukumu la kulea watoto linakuwa gumu kwao.

Wasikilize wanafamilia hao wakitoa wito wao kwa serikali;

Kwa mujibu wa Katibu wa Mambo ya Nje wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa, Aprili 5 mwaka huu magari mawili yenye namba za usajili Z 941 EG na Z 229 EQ yalivamia Vijiji vya Mitambuuni na Makoongeni katika Jimbo la Mtambwe  wilayani Wete, Pemba na kutoweka na vijana sita.

Vijana hao sita waliotekwa walikuwa ni Thuwein Nassor Hemed (30), Khamis Abdalla Mattar (25), Juma Kombo Fimbo (17), Said Sanani Mohamed (16), Khalid Khamis Hassan (30) na Abdallah Khamis Abdallah (19).

Aidha, baada ya siku kadhaa vijana watatu ambao ni Said Sanani Mohammed, Juma Kombo Fimbo na Abdallah Abdallah walipatikana huku wengine wakiwa bado hawajulikani walipo.