BAADA ya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wolaita Dicha ya Ethiopia, wachezaji wa timu hiyo wamesema hizo ni salamu kwa timu za Ligi Kuu Bara, ikiwemo Simba ambayo kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi hiyo kwani yenyewe inahitaji kutetea ubingwa wake.
Nyota hao wametamba kuwa kuanzia sasa hawataacha nyuma pointi yoyote katika mechi zote watakazocheza.
Juzi Jumamosi, Yanga ikiwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, iliibuka na ushindi huo ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wachezaji wa Yanga ambao keshokutwa Jumatano watakuwa na kibarua kingine cha kuhakikisha wanapata pointi tatu mbele ya Singida United ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara, wamesema kuwa, kuanzia ushindi dhidi ya Wolaita Dicha, hawataacha pointi hata moja kwenye michuano yote wanayoshiriki kwa sasa.
Timu hiyo ambayo kwenye ligi kuu inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 46 kabla ya mchezo wa Azam jana Jumapili dhidi ya Mbeya City, Aprili 18, mwaka huu inatarajiwa kurudiana na Wolaita Dicha huko nchini Ethiopia.
Akizungumza na Championi Jumatatu, beki wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’, alisema: “Unajua baada ya kufungwa na Singida na kuondolewa katika Kombe la FA, wapinzani wetu waliongea sana, sasa tukajipanga na kusema tutawaonyesha kitu.
“Hivi sasa tulivyo ni kama mnyama aliyejeruhiwa, tukikutana na timu yoyote mbele ni kipigo tu, kuachwa pointi tatu na Simba huku tukiwa michezo sawa si kitu cha ajabu, tutawashangaza wengi mwisho wa msimu.”
Msimu uliopita, Simba iliongoza kwa muda mrefu na kuna wakati kabla ya mechi tatu za mwisho za mzunguko wa kwanza, Simba walikuwa wanaongoza kwa tofauti ya pointi nane lakini walikamatwa na mwisho Yanga wakachukua ubingwa kwa tofauti ya mabao baada ya timu zote kuwa na pointi 68.
Hata hivyo, msimu huu Simba imefunga mabao mengi zaidi ya Yanga na kama wakilingana pointi, basi Wekundu wana nafasi kubwa ya kushinda.