Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amesema anatamani kuona Wakristo na Watanzania wote wanavaa ujasiri na kuwa na sauti ya kuonya kwa kusema watu wamuogope Mungu kwa maovu yanayofanyika.
Askofu Shoo amesema kuwa, watu wenye midomo michafu, waliojaa viburi na unafiki mkubwa ambao hawaoni madhaifu yao ni vema Watanzania na Wakristo wakaungana katika kutoa maonyo dhidi ya watu hao kwa lengo la kuwafanya watu wote waishi kwa amani bila hofu.
Aliyasema hayo jana Jumapili Aprili 8, wakati akiongoza ibada katika Usharika wa Msaranga, mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Askofu Dkt Shoo ambaye pia ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini alisema kwamba dunia hii imejaa watu wa aina mbalimbali ambapo wame waliokata tamaa, wasiosikia maonyo, wenye viburi, hivyo ni vyema Watanzania na Wakristo wakasimama pamoja na kuwaonya watu hawa dhidi ya madhaifu yao.
“Kanisa linatamani kuona Watanzania wanaishi katika hali ya amani, upendo, mshikamano, maelewano pasipo kujali vyeo vyao wala itikadi zao za kisiana na ubaguzi wa kikabila na ukanda,” amesema.
Dkt Shoo amesema kuwa kuna watu wamekuwa wakidai wanahubiri maneno yenye amani lakini wanayoyasema hayaendani na matendo yao, hivyo watanzania na wakristo wana wajibu wa kusimama na kuhubiri amani ya kweli kwa vitendo.