Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitoa ufafanuzi wa uwapo wa upepo mkali, Shirika la umeme Tazania (TANESCO) limeeleza sababu nne za kukatika kwa nishati hiyo wakati wa mvua.
TMA ilisema upepo ulioambatana na mvua juzi saa tano usiku jijini Dar es Salaam na kusababisha maeneo mengi kutokuwa na umeme, ulisababishwa na kimbunga kinachoitwa Dumanzile.
Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Leila Muhaji alisema kukatika kwa umeme wakati wa mvua husababishwa na vikombe vilivyopo kwenye nguzo wakati wa kiangazi kujaa vumbi na mvua inaponyesha hutengeneza njia hivyo kuwapo hitilafu ya umeme.
Leila alisema sababu nyingine ni miundombinu ya umeme kuwa imepita kwenye makazi ya watu ikiwamo ardhini, hivyo wakati wa kiangazi haionekani na baadhi ya wananchi hulima au kupitisha mifugo na kusababisha nyaya kuchunika.
“Mvua ikinyesha inakuwa rahisi kupita kwenye miundombinu na kusababisha hitilafu ya umeme kwenye eneo linalolimwa au kupitisha mifugo,” alisema Leila.
Alisema sababu nyingine ni upepo unaosababisha nyaya kucheza na kugusana hivyo kukatika na hitilafu kutokea.
Aliongeza kuwa miundombinu ya umeme kuwa ya muda mrefu imekuwa moja ya sababu ya kutokea kwa tatizo hilo.
Hata hivyo, Leila alisema Serikali imeanzisha miradi ya umeme ikiwamo uboreshaji wa upatikanaji wa nishati unaoendana na ukuaji na ongezeko la watu uliozinduliwa mwaka 2016 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema serikali imehakikisha miradi hiyo inafanyika maeneo mbalimbali nchini na kwa Jiji la Dar es Salaam vituo kadhaa vimefunguliwa vya kupoozea na kusambaza umeme, vikiwamo vya Kipawa, Mbagala na Chang’ombe.
Kuhusu upepo na mvua, TMA ilisema kimbunga katika Bandari ya Hindi kiitwacho Dumanzile kimesababisha hali hiyo huku upepo ukivuma kilomita 40 kwa saa.
Meneja ueneshaji wa vituo vya hali ya hewa, Hellen Msemo aliitaja mikoa yenye msimu wa mvua za masika itakayoathiriwa na kimbunga hicho kuwa ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro, Lindi na Mtwara.
Msemo aliwashauri watumiaji wa Bahari na wakazi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari na hatua stahiki. Alisema TMA itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.
Kutokana na upepo wa juzi, paa za nyumba eneo la Makoka jijini Dar es Salaam ziliezuliwa. Mo