Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, meneja wa soko la wafanyabiashara wadogo la Machinga Complex lililoko jijini Dar es Salaam, Nyamsukura Masondore, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Akimsomea hati ya mashtaka inayomkabili mshtakiwa huyo jana Ijumaa Machi 9, 2018, kwa Hakimu Mkazi Adelf Sachore, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Sophia Gura alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo tarehe tofauti kati ya Septemba 29 na Oktoba 7, 2014 akiwa mwajiriwa wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama meneja wa jengo la biashara la Machinga Complex.
Sophia alidai kuwa Masondore akiwa na jukumu la kuongoza shughuli za kila siku za jengo hilo, kwa makusudi alitumia vibaya madaraka yake kwa kutoa eneo ambalo halijaidhinishwa kwenye jengo hilo kwa Umoja wa Wauza Mitumba.
Imedaiwa kufanya kwake hivyo ni kinyume na kanuni namba 12(a) na (b) za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam( Bodi ya Huduma ya Jengo hilo) na kwamba kutokana na kitendo hicho mshtakiwa huyo alijipatia faida yeye pamoja na wengine.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.
Hata hivyo, wakili anayemtetea, Jamhuri Johnson ameiomba mahakama impatie dhamana mteja wake huyo na upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi.
Hakimu Sachore alitoa masharti ya dhamana akimtaka Masondore kuwa na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho kutoka taasisi zinazotambulika kisheria na pia watasaini ahadi ya Sh 5 milioni. Na kwamba barua hizo zitahakikiwa.
Kesi imeahirishwa hadi Machi 20, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.