SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 8 Machi 2018

T media news

Serikali ya Kenya ‘yafilisika’

Waziri wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich amesema kuwa serikali ya nchi hiyo haina fedha na hivyo inakumbana na changamoto kubwa kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Waziri huyo amesema kuwa, kuna mpango wa kupunguza bajeti zilizotengwa kwa ajili ya kaunti 47 za nchini hiyo.

Aliyasema hayo jana katika kikao cha fedha cha kamati ya seneti ambapo aliwaambia maseneta wapunguze bajeti za kaunti hadi kufikia Ksh 18 bilioni (TZS 400.7bn) katika mwaka huu wa fedha.

Akitaja sababu zilizopelekea hali hiyo, Waziri Rotich  alisema kuwa ni mchakato wa uchaguzi ni moja ya sababu, lakini pia changamoto za kisiasa pia zilipelekea taifa kutumia fedha nyingi, na biashara nyingi zilifungwa kutokana na tishio la usalama.

Amesema kuwa, wamezungumza na Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA) ili kuona ni namna gani wataweza kukabili changamoto hizo.

Baadhi ya magavana wamesema kuwa, kupunguzwa kwa bajeti za kaunti kunaweza kuathiri miradi ya maendeleo ambayo tayari imeshaanza kutekekelezwa.

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limesema kuwa ukuaji wa  uchumi wa Kenya inatarajiwa kuporomoka hadi 4.8% kutoka 5.8% iliyokuwapo mwaka 2016 kutokana na vurugu za kisiasa na ukame.