SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 17 Februari 2018

T media news

Waziri Mkuu Akemea Vitendo Vinavyoharibu Ubora Wa Pamba .....Awataka Wasiweke Mchanga Wala Maji Ili Kuongeza Uzito

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa pamba kutochanganya pamba na mchanga au maji kwa sababu watakosa wanunuzi.

Pia amesema Serikali itapambana na watu wote wanaotaka kuvuruga zao hilo, hivyo amewataka wakulima waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Waziri mkuu alitoa kauli hiyo jana (Ijumaa, Februari 16, 2018) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Kwimba.

“Wakulima msichezee pamba kwa kuichanganya na chochote ili kuiongezea uzito kwa sababu mtaharibu sifa nzuri ya pamba ya Tanzania ndani nan je ya nchi.”

Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakulima wasiokuwa waaminifu ambao kabla ya kuipeleka pamba sokoni wanachanganya na maji au mchanga.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kuona tija tangu ilipoagiza Maofisa Kilimo katika mikoa inayolima pamba wasimamie kilimo hicho kuanzia ngazi za awali.

Akizungumzia kuhusu suala la wanunuzi wa pamba, Waziri Mkuu alisema tayari Serikali imeweka mikakati ya kutosha itakayowezesha pamba yote kununuliwa.

Kuhusu suala la bei alisema wataangalia katika soko la Dunia na kisha watawashawishi wanunuzi wanunue kwa bei nzuri itakayowanufaisha wakulima.

Alisema Serikali itaendelea kusimamia zao hilo kuanzia hatua za maandalizi ya shamba kwa kulima kitaalam, upatikanaji wa pembejeo hadi masoko.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea mashamba ya mfano ya pamba katika kijiji cha Kilyaboya na Igumangobo ambapo alisema ameridhishwa mashamba hayo.

Pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Kadashi, mradi ambao ulioibuliwa na Diwani wa Kata ya Maligisu, Bw. Tabu Mapembe.

Kata ya Maligisu yenye vijiji vine ina zahanati moja tu, kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo kutasaidia kupunguza tatizo la utoaji wa huduma za afya.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAMOSI, FEBRUARI 17, 2018.