Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amemaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya wananchi wa kijiji cha Utete wilayani Rufiji mkoani Pwani na hifadhi ya msitu wa Kale baada ya kuwapa wananchi eneo la kilimo na makazi.
Dk Kigwangalla ametoa uamuzi huo jana Februari 15, 2018 alipotembelea kijiji hicho na hifadhi hiyo ambayo baadhi ya maeneo yake yalikuwa yakitumiwa na wananchi kwa shughuli za kilimo.
“Nimeona hakuna madhara yoyote iwapo tutamega eneo kidogo katika msitu wa kale ambako wananchi wamekuwa wakifanya shughuli zao za kilimo na kuwapa ili waendelee kujipatia riziki, ”amesema Dk Kigwangalla.
Amebainisha kuwa mbali na eneo hilo pia eneo la chemichemi ambalo lilivamiwa na wakazi hao, iangaliwe namna ya kuhamisha mipaka na kuwaacha wananchi nje ya hifadhi bila kuathiri chemichemi hiyo ili waendelee na maisha yao.
Katika kuhakikisha jambo hilo linafanyika, Dk Kigwangalla amemwagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Profesa Dos Santos Silayo kuunda timu ya wataalamu itakayoshirikiana na wataalamu wa mkoa na wilaya kusimamia mgawanyo wa ardhi kwa wananchi na hifadhi za Taifa.
Amesema mchakato huo utakaofanywa na wataalamu hao utakuwa wa kisheria ili kuwapa haki ya kudumu wananchi hao hata anapokuwa hayupo katika nafasi hiyo.
“Lazima sheria zirekebishwe ili muishi na kulima kihalali, nisipolifanya kisheria nikiondoka anaweza kuja mwingine kuwasumbua, sheria zitafuatwa za kuhamisha mipaka,” amesema.
“Ombi la Mbunge wenu (Mohamed Mchengelwa) lilikuwa kwa wakulima wazawa, naomba wabaki wale wale na si muwaite wawekezaji kutoka mjini waje kulima, hata wazee ombi lenu lilikuwa ni kwenye mashamba yale ya asili,” amesema Dk Kigwangalla.
Amesema amechukua jukumu hilo ili kuhakikisha wananchi wanamaliza mgogoro na hifadhi hiyo ambayo inabaki na eneo lake.