RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa amewataka wadau mbalimbali na wananchi kuendelea kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo nchini ambapo zaidi ya sh.milioni 200 zilipatikana.
Mkapa alitoa ombi hilo wakati akiongoza harambee ya kuchangia mfuko huo iliyofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya nje na ndani pamoja na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
“Ni wajibu kwa kila mwananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia mfuko huu ili kusaidia mapambano ya Ukimwi hapa nchini na kuwa mapmbano hayo si ya mtu mmoja” alisema Mkapa.
Katika hatua nyingine Rais Mstaafu Mkapa ameiomba Serikali kuendelea kutenga fedha za Ukimwi katika bajeti zake.
Akizungumza katika harambee hiyo Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema kwamba Serikali itaendelea kusimamia Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) katika matumizi ya fedha hizo.
Mhagama alisema asilimia 60 ya fedha hizo zitatumika kununulia madawa, asilimia 25 itatumika katika kutoa huduma za kinga pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya Ukimwi na asilimia 15 zitatumika kwa ajili ya uwezeshaji na ufuatiliaji wa programu za Ukimwi.
Mhagama aliongeza kuwa matumizi ya dawa za kufubaza VVU kwa wanawake ni asilimia 92.9 wakati wanaume ni 86.1 na kuwa katika tisini ya tatu kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15-64 ambao wametoa taarifa kuwa wanatumia dawa za kufubaza VVU asilimia 87.7 ya watu hao inaonyesha kiasi cha VVU kimefubazwa wanawake ni asilimia 89.2 na wanaume ni asilimia 84.
Alisema utafiti huo pia umeonyesha kuwa maambukizo mapya ya VVU (HIV incidence) kwa mwaka kwa watu wenye umri wa miaka 15-64 Tanzania Bara ni asilimia 0.29 ambayo ni sawa na watu 81,000.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko huo, Bw. Godfrey Simbeye alisema sekta binafsi imeunga mkono kwa kiasi kikubwa katika kuchangia mfuko huo na kuwa hakutakuwa na matumizi mabaya ya fedha hizo na zitakwenda kutumika kwa kile kilichokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko alimshukuru Rais Mstaafu Mkapa kwa kukubali kushiriki kuongoza harambee hiyo na kueleza kuwa Tacaids imekuwa ikiendesha harambee mbalimbali pamoja na kuandaa mashindano ya michezo na viingilio vyake vimekuwa vikiingia katika mfuko huo.