Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imejibu hoja mbili kati ya 14 zilizowasilishwa kwake na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) huku ikisisitiza kuwa hoja zingine 12 hazimo ndani ya mamlaka yake.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe amesema tume kwa kutoa kauli hiyo, inakwepa wajibu wake na kuwa sehemu ya serikali.
Katika mkutano wake na vyama vya siasa jijini Dar es Salaam jana uliohudhuriwa na vyama 17 kati ya 19, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi, NEC ilisema imeamua kuuitisha kwa lengo la kupeana taarifa na kujadiliana mambo mbalimbali na uchaguzi mdogo katika majimbo matatu na madiwani katika kata sita Tanzania Bara.
Majibu ya hoja za Ukawa yalitolewa baada ya mchangiaji wa mada, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Juju Danda, kuhoji juu ya barua hiyo huku akiituhumu tume kunyamaza na kutoitisha mkutano wa wadau kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo.
"Ukawa tuliomba kukutana na wadau wote pamoja na tume kabla ya uchaguzi, lakini sasa mmetuita, mmeshapanga tarehe ya uchaguzi," Danda alisema.
"Wasimamizi wa uchaguzi ni makada, tunakwenda kushindana kwenye uchaguzi wa nini wakati mshindi anajulikana?” Danda alihoji.
Baada ya hoja hiyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, alitoa barua ya Ukawa na kueleza kubainisha kuwa iliwafikia Desemba 14 na waliijibu siku nne baadaye na kurejesha majibu kwa aliyeiandika.
"Mwandishi wa barua ndiye alijibiwa, fuatilia kwenye vyama vyenu, aliyeandika alipata jibu na alijulishwa kwa maandishi, alitakiwa kufika leo kwenye kikao ili yaliyomo kwenye barua yaweze kujadiliwa, lakini hajafika,” alisema Jaji Kaijage.
Mwenyekiti wa NEC huyo alijibu hoja moja baada ya nyingine zilizowasilishwa kwao na Ukawa kupitia barua hiyo akibainisha kuwa hoja yao ya kwanza na ya pili ndiyo ziko ndani ya mamlaka ya tume, akianza na hoja ya kutolewa nje kwa mawakala wa uchaguzi na kuzuiwa kwa mikutano ya siasa nchini.
“Niwasihi sana viongozi wa vyama vya siasa, makosa yoyote yanayokiuka taratibu za kisheria, za kiuchaguzi, taratibu muhimu zinazomnyima mgombea haki ya kugombea na kupitishwa yafuate mkondo. Sheria na taratibu zetu hazijaacha ombwe, foramu imewekwa ya kuwasilisha tatizo hilo, hakuna sababu yoyote ya msingi kwa wakala kutolewa nje,” alisema na kueleza zaidi:
“Wakala anapotolewa maana yake uchaguzi haujaenda vizuri, na sheria imeweka utaratibu wa wapi malalamiko yapelekwe ili ufumbuzi upatikane."
Mwenyekiti wa NEC huyo alisema kama kuna wakala alitolewa nje, uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria za nchi, maadili, taratibu na kanuni.
Jaji Kaijage alisema hoja ya pili ni madai ya Ukawa kuwa matokeo halisi hayatangazwi akifafanua kuwa kifungu cha 81 cha Sheria ya Uchaguzi na kifungu 82 cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vinaeleza anayetangazwa kuwa mshindi ni ambaye amepata kura nyingi halali zaidi ya mwingine.
“Lalamiko la msingi kuwa matokeo halisi kutotangazwa, pengine ambaye siyo mshindi ndiye katangazwa, hili ni kosa kubwa sana. Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Serikali za Mitaa imeweka wazi kwamba malalamiko yenye ushahidi wa msingi ya kukiuka sheria na taratibu, ana haki ya kwenda mbele ya vyombo vya sheria kulalamika na ikithibitika uchaguzi unatenguliwa,” alisema na kuongeza:
“Laiti kama haya na mengine yangewasilishwa katika mamlaka za kisheria na kanuni yangekuwa yamepata majibu. Kusita au kukataa kwa sababu nyingine ndiyo kunaleta malalamiko. Tulishasema malalamiko yote yaliyopo humu (barua) hakuna ambalo haliwezi kushughulikiwa chini ya sheria za nchi."
Kuhusu kupigwa marufuku kwa mikutano ya vyama vya siasa, Jaji Kaijage alisema majukumu ya NEC yako kwenye katiba na sheria, hivyo ni suala ambalo haliko kwenye mamlaka ya tume na wanabaki kuwa wasikilizaji pekee.
Alisema hoja ya tatu ya Ukawa ni kuwapo kwa mauaji nchini ambayo alikiri kuwa ni tatizo na ni kosa kubwa la jinai, lakini akasisitiza kuwa halipo ndani ya majukumu ya NEC.
“Tume kuitisha kikao cha kujadiliana kuhusu mauaji tunaweza kushtakiwa kwa kuparamia mamlaka na madaraka ambayo tume haina," Jaji Kaijage alieleza.
Alibainisha kuwa hoja ya nne ya Ukawa ni madai ya kuminywa kwa vyombo vya habari, akieleza kuwa suala hilo pia lipo nje ya mamlaka yao na kwamba linaweza kuwaingiza kwenye matatizo.
"Uchaguzi hauwezi kutenguliwa na huwezi kuitisha kikao kujadili mambo ambayo tume haina mamlaka nayo," alisema.
Aliitaja hoja ya tano kuwa ni vituo kuvamiwa wakati wa kuhesabu kura akifafanua kuwa vifungu na maelekezo yametolewa vizuri kabla ya kuanza upigaji wa kura na wakati wa kufunga kituo kuna fomu maalum inajazwa kama kuna malalamiko yoyote yanaainishwa.
Alisema kama tatizo lilijitokeza, kanuni na taratibu zinaweka wajibu kwa msimamizi wa kituo kutoa ufafanuzi, kama hakutoa inakuwa ndiyo msingi wa kupeleka kwenye mamlaka za kisheria.
Jaji Kaijage alisema hoja zingine za Ukawa ni kutaka kuwa na tume huru, katiba mpya, mikutano ya hadhara, maandamano na kutofanya kazi za kisiasa.
"Sisi kama Tume tunafuata Katiba, sheria zilizopo, kanuni, suala la kikatiba tunajiuliza hivi tume inayo mamlaka ya kufanya marekebisho ya sheria au kuhitisha mkutano wenye lengo la kuweka sawa katiba inayolalamikiwa," Jaji Kaijage alisema na kuongeza:
"Tume inaweza ikatoa ufumbuzi juu ya kuruhusiwa au kutoruhusiwa kwa mikutano ya hadhara?
"Kuhusu katiba mpya, sisi tunaweza tukatoa maoni kama watu wengine mbele ya chombo kilichokabidhiwa jukumu la kufanya marekebisho ya katiba au sheria."
Alisema lawama kwa tume ni zinapaswa kuwa kushindwa kutekeleza mamlaka yake, kanuni na sheria zinazoongoza uchaguzi.
“Tume iko makini kuhakikisha inafuata taratibu zote za kisheria, kanuni na kimaadili. Tume itakuwa ya mwisho kukiuka sheria, taratibu na katiba ya nchi,” alisema.
Katika mkutano huo, baadhi ya wajumbe waliitaka tume kutokukwepa majukumu yake kwa kuwa ndiyo chombo mama na kwamba siyo dhambi kuishauri serikali pale wanapoona wana nafasi ya kufanya hivyo.
“Mtu anafika kituoni na mapanga anakata watu, ukilalamika unaambiwa ni suala la polisi. Tume haichukui hatua, unatuambie tukaelimishe wananchi, lakini wanajua wamezuiliwa kufanya mikutano, kazi yao ilikuwa ni kuelimisha jamii,” alisema mmoja wa wajumbe waliohudhuria mkutano huo.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhani, aliwasilisha taarifa ya maandalizi ya uchaguzi mdogo katika majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea mjini na kata sita, akibainisha kuwa Chadema na NCCR- Mageuzi wamesusa.
Mbowe Afunguka:
Akizungumza jana, Mbowe alisema katika mambo yanayohusu uchaguzi na maisha ya watu, hakutakiwi kuangalia kama lipo ndani ya mamlaka au la, bali kinachotakiwa ni kushauriana.
“Kuna mambo kadhaa wanajadiliana, jambo linahusu idara nyingine na kuishauri ni mambo ya kawaida katika uongozi, NEC kama mhusika mkuu wa uchaguzi, watendaji wengine wa idara za serikali wanapofanya mambo yaliyo kinyume ni wajibu wao kukemea,” alisema.
Mbowe alisema polisi wanapoumiza wafuasi wa chama fulani katika uchaguzi ni ngumu kusema NEC haihusiki na wanaohusika ni polisi pekee. Alisema wajibu wao ni kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki kwa njia zote za amani na haki.
“Jambo lolote linapoibuliwa halijadiliwi kwenye mkutano wa waandishi wa habari, bali wadau wakiwa na kikao cha ndani. Tuliwaandikia tukutane na NEC, polisi, usalama wa taifa na Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alidai uchaguzi mdogo uliopita ulikuwa na kasoro mbalimbali zinazolalamikiwa na wadau, lakini inashangaza tume kusema haikuona tatizo.
Kiongozi huyo wa Ukawa pia alidai kikao kilichofanyika jana kilipangwa kufanyika mapema zaidi lakini kikaahirishwa na kwamba Chadema hawakupata barua ya tarehe mpya ya kikao.
“Tulikuwa Nairobi, Kenya kwa ajili ya kumsafirisha Tundu Lissu. Kikao kiliitwa mwezi uliopita, kikahairishwa japo hawakueleza agenda za kikao. Taarifa za uwapo wa mkutano mimi (Mwenyekiti), Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu hatuna taarifa,” alisema na kuongeza:
“Tuna wajibu wa kuhakikisha nchi inakuwa na uchaguzi wa haki amani, kila mmoja aone faida ya vyama vya siasa na siyo hasara.
“Tatizo lililopo, tume inajiona wao ni serikali, wanatuangalia kama watu wa kupambana nao, kukinzana na hoja na siyo watu wa kushirikiana kutafuta suluhisho. Ndiyo maana kila tukilalamika wanajenga ‘defence’ (kujilinda), wameegemea upande wa serikali.
“Ni bahati mbaya sana iliyopo nchini kwamba vyombo vyetu vya kusimamia mambo ya kuleta umoja katika taifa wanaanza kuwa sehemu ya vyama, wanashiriki upande mmoja na kukandamiza haki ya upande wa pili na wanadanganya umma kuwa haki inatolewa kumbe haitolewi."
Awali wakati wa mkutano Mwakilishi wa ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa, alisema Chadema hakikufika kushiriki kwa kuwa imekuwa kawaida kuzungumza lakini mambo hayashughulikiwi.
“Jeshi la Polisi linatumika vibaya, magari ya polisi maana yake wapinzani wasijitokeze watakamatwa, kwanini polisi wanaenda na magari yenye bendera nyekundu, mavazi ya kutisha wananchi?" Alihoji.
Aliitaka tume kuacha kuwatumia wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi na wakuu wa wilaya na mikoa kuacha kufanya siasa.
“Unakuta RC na DC ambao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama wanafanya kampeni za CCM. Ndiyo maana tunasema wapeni ushindi CCM waendelee kutawala, hakuna haja ya kufanyika uchaguzi,” alisema Mtemelwa.
Katibu Mkuu wa Sau, Jonson Mwangosi na Lulu Kimwaga wa Tadea, waliiomba tume kusaidia vyama visisivyo na uwakilishi bungeni vipate ruzuku ili viweze kushindana kwenye chaguzi mbalimbali.
“Uchaguzi wa sasa ni sawa na kumpa nyama kibogoyo ashindane na mwenye meno," alisema Kimwaga.
Mwezi uliopita Ukawa kupitia kwa Mbowe ulitangaza kususa kushiriki uchaguzi mdogo wa majimbo matatu na kata sita uliopangwa kufanyika Jumamosi ukitaka uitishwe kwanza mkutano wa NEC na wadau wa uchaguzi kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi mdogo wa madiwani wa kata 43 Tanzania Bara uliofanyika Novemba 26.