Na Dr. Mabula
Kuna watu katika jamii wana umri mkubwa sana, lakini sura bado zinaonekana kung’aa mithili ya vijana. Jambo hili halitokei kwa bahati tu, bali kuna mambo ya msingi ya kuzingatia katika mfumo mzima wa maisha yako.
Hapa chini ni mambo 9 inayotakiwa kuzingatia ili kuweza kuishi maisha marefu na uwe na afya njema. Usiishie tu kwenye haya yaliyojadiliwa hapa, bali unaweza ukaongeza mengine unayoona yana manufaa kwako. Haya yamewekwa kukupa mwanga tu wa kuanzia.
1. Kuushughulisha mwili mara kwa mara kwa mazoezi au kazi za kila siku. Ikiwa una kazi ya kukaa ofisini muda mrefu ni vyema kufanya mazoezi baada ya kazi zako.
2. Kuwa na kusudi katika maisha yaani sababu ya kukufanya uamke kila siku asubuhi. Wajapani wanaoishi miaka mingi wanaita “IKIGAI” likiwa na maana ya “sababu ya kuwa hai.
3. Kupunguza mkazo (stress) kwenye maisha yako, ina maana kuweza kuwa na wakati wa kila jambo mfano kujumuika na wengine kanisani, kwenda kupunga upepo ufukweni, kukutana na marafiki kuzungumza n.k!
4. Kula chakula kwa kiasi sio mpaka ushibe kabisa. Neno “Hara hachi bu” la kikonfyushasi (falsafa na maadili ya Kichina) lina maana kula chakula kidogo ushibe kwa angalau 80% na sio kushiba 100%.
5. Kuweka kipaumbele kwenye vyakula vya mimea (mbogamboga na matunda) unaweza kula nyama, samaki na maziwa ila kwa kiwango kidogo. Vyakula vya mimea hupunguza hatari ya saratani, maradhi ya moyo, kisukari n.k!
6. Kunywa vileo kistaarabu. Watafiti wanadai wanywaji pombe kistaarabu huishi umri mkubwa kuliko wasiokunywa kabisa, pia wamedai wanywaji pombe kistaarabu wanapunguza hatari ya kupatwa na maradhi ya moyo.
7. Kujihusisha na makundi ya kijamii yanayohamasisha afya bora mfano vikundi vya mazoezi, vikundi vya kucheza muziki n.k!
8. Kushiriki na wengine kwenye vikundi vya kidini vyenye utendaji wa mara kwa mara mfano vikundi vinavyotembelea watu sehemu mbalimbali wanapopatikana na kuwahubiria kuwafundisha habari za Mungu.
9. Kuimarisha mahusiano ya kifamilia pamoja na ndugu wengine. Kuwa na ukawaida wa kuwasiliana, kukutana na kushirikiana utendaji mbalimbali kutia ndani sherehe na misiba.