SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 8 Januari 2018

T media news

Serikali Yataifisha Tani 65 za Samaki zenye Thamani ya Milioni 300

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina amekamata kilo 65600 za samaki wachanga aina ya Sangara waliokaushwa kwa chumvi wenye thamani ya shilingi milioni mia tatu katika Kisiwa cha Lubili wilayani Muleba kwenye Mkoa wa Kagera baada ya wamiliki wa samaki hao kukimbia.

 

Akizungumza jana na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya  Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera, Mpina alisema  tukio la kukamatwa kwa samaki hao lilifanikiwa baada ya yeye kupata taarifa kutoka  kwa raia mwema ambapo aliagiza mamlaka za Wilaya ya Muleba kufuatilia kwa karibu hatimaye kuwakuta  samaki hao wakiwa wameanikwa chini katika kisiwa hicho.

 

Waziri  Mpina alisema Sheria ya Uvuvi namba 22 ya Mwaka 2003  na Kanuni zake za mwaka 2009 kifungu cha 90(1) inataka samaki wanaovuliwa waandaliwe katika mazingira yanayokidhi vigezo vya usalama  kwa mlaji na  kwamba ni kosa kisheria kuwavua au kuchakata samaki aina ya Sangara walio chini ya sentimeta 50 kwa kuwa ni wachanga na sentimita 25 kwa Samaki aina ya Sato. Pia sentimita 85 kwa Sangara kwa kuwa ni wazazi wanaotakiwa kundelea kuzaa.

 

Aidha Waziri aliongeza kwamba Sheria hiyo imetoa  mamlaka kwa watendaji wa Serikali kutaifisha mali zote zilitumika katika uvuvi haramu kupitia  kifungu cha 37(a) (ii) na (iii) pamoja na   Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu namba 29 ya mwaka 1994.

 

Waziri Mpina  ameagiza  watendaji kufuata taratibu zote za kisheria ili samaki hao wauzwe kwa njia ya mnada  na mapato hayo yaingie Serikalini mara moja.Aidha  aliwaonya wafanyabiashara na wavuvi kuachana na uvuvi haramu kwa kuwa ni kuhujumu raslimali za taifa  ambazo zingetumika kwa kizazi cha sasa  na baadaye.

“Mfanyabiashara yoyote wa samaki na mazao yake anayetaka kufilisika  na kutafuta matatizo katika maisha yake aendelee na biashara ya uvuvi haramu”alisisitiza Mpina

 

Kufuatia tukio hili, Waziri Mpina  amewapa wiki mbili wafanyabiashara na wasafirishaji wote wa samaki na mazao yake waliopewa leseni  ya kufanya  biashara hiyo kwa mwaka 2018 kuleta cheti cha uthibitisho cha ulipaji kodi ambapo amesema kama watashindwa kufanya hivyo hawataruhusiwa kufanya biashara hiyo.

 

Alisema kuanzia sasa wafanyabiashara wote wote wataruhusiwa  kupata leseni hiyo baada ya kuwasilisha cheti cha uthibitisho wa ulipaji kodi, cheti cha usajili wa kampuni na mahesabu ya kibiashara  yaliyohakikiwa ili kuepuka utaratibu wa sasa ambao unatoa mwanya kwa mawakala wa ndani na nje ya nchi kujiingiza katika biashara hiyo kinyemela  na kuikosesha Serikali mapato kwa  kukwepa kulipa kodi mbalimbali.

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustapha Kijuu alisema  Serikali  itahakikisha kwamba uvuvi haramu unakuwa historia katika Mkoa wa Kagera na kuwataka wananchi kuwafichua wavuvi  haramu  ili vyombo vya Serikali viwakamate na kuwafikisha katika  mikondo ya sheria.

 

Alisema  sekta ya uvuvi inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa  katika kuinua hali ya uchumi kwenye mkoa wake na taifa kwa ujumla kama  wadau wote watashiriki kikamilifu katika  vita dhidi ya  uvuvi haramu ambapo alisema  jumla ya wananchi 26,272 wameajiriwa kutokana na shughuli za uvuvi katika mkoa huo.

 

Alisema mkoa utaendelea na kupambana na uvuvi haramu ambapo  kwa mwaka 2016/17 jumla ya doria 65 zilifanyika na kuwezesha kukamatwa kwa makokoro ya Sangara 422, nyavu ndogo za dagaa 57,nyavu za timba 3,231, nyavu za makila 14,141, ndoano 711, katuli 16,mitumbwi 133 samaki wachanga kilo 5,621 na watuhumiwa 86.

 

Hata hivyo Mkuu  huyo alisema  katika kuongeza uzalishaji wa samaki jumla ya mabwawa 584 yamechimbwa kwa mwaka 2016/2017 kutoka mabwawa 181 mwaka 2005/2006 sawa na ongezeko la mabwawa 403.

 

Kwa upande mwingine Mkuu wa Mkoa alisema hivi karibuni Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara ilikamata gari lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi Canter likiwa limepakia samaki kilo 2,000 aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato kwenye mpaka wa Murusagamba wilayani Ngara.

 

 Alisema Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana  Ayoub Ngoma na dereva  wa gari hilo Ayoub Sanga  walishikiliwa na polisi kwa hatua za kisheria kwa tuhuma za  kushiriki katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/= ambapo Ngoma

ameshasimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

 

Pia Mshauri wa Uvuvi wa Mkuu wa Mkoa, Efrazi Mkama na  maafisa Uvuvi wa Halmashauri ya Muleba Wilfred Tibendelana na Maengo Nchimani na Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba vijijini Renus Ruhuzi wanaendelea kuripoti katika kituo cha polisi Bukoba kwa mahojiano ya kisheria juu ya utoroshwaji wa samaki hao.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Mwanaidi  Mlolwa alisema Serikali ina mkono mrefu  na kwamba  hakuna mtu atakayebaki salama iwapo atajihusisha  na uvuvi haramu.

 

Aidha alisema maafisa uvuvi wanawajibu wa kuhifadhi na kutunza takwimu mbalimbali za sekta ya uvuvi ili kutoa picha halisi ya jinsi sekta inavyochangia katika uchumi wa nchi kwa ujumla.

 

“Kimsingi sekta ya uvuvi ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa takwimu sahihi