SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 9 Januari 2018

T media news

Naibu Waziri Mpya wa Madini, Doto Biteko aanza kazi

Naibu Waziri wa Madini, Doto Mashaka Biteko ambaye ameapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Madini tarehe 8 Januari, 2018 ameanza kazi rasmi kwa kufanya kikao na Viongozi na Watumishi wa Wizara husika.

Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Wizara jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu, Profesa Simon Msanjila.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri huyo alieleza kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya viongozi na watumishi wa Wizara ili kwa pamoja wasimamie ipasavyo Rasilimali Madini na kuhakikisha kuwa inafaidisha Taifa.

“Ili kutimiza malengo ya Rais wetu ya kuhakikisha kuwa Rasimali Madini inaendelezwa ipasavyo, hatuna budi kushirikiana na kushikamana ili kuwe na umoja utakaoleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu kwani sisi sote ni watumishi wa watanzania,” alisema Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa Uteuzi wa Naibu Waziri wa Pili katika Wizara ya Madini unaonesha namna Rais John Magufuli anavyoichukulia kwa umuhimu wa pekee Sekta ya Madini ambayo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Tutashirikiana kwa pamoja na watumishi wa Wizara ili kuweza kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa mbele zaidi,” alisema Nyongo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema kuwa viongozi hao na watumishi kwa pamoja watafanikisha mategemeo na malengo ya Rais John Magufuli ya kuhakikisha kuwa Rasimali Madini inalinufaisha Taifa.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaeleza watumishi kuhusu uamuzi wa Rais John Magufuli wa kutengua uteuzi wa Kamishna wa Madini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka na kumteua Profesa Shukrani Elisha Manya kuwa Kamishna wa Madini na pia kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini na hivyo kuwaasa watumishi kumpa ushirikiano Kamishna huyo mpya.