SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 10 Januari 2018

T media news

Mbowe Nae Kazikana Kauli za Lowassa Kwa Rais Magufuli....Kasema Huo Sio Msimamo wa CHADEMA, Ni Mawazo Yake Binafsi

Baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa kumtembelea Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya nae mazungumzo, Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe amesema kuwa kile kilichosemwa na Lowassa  sio msimamo wa CHADEMA bali ni mawazo yake binafsi.

Akizungumza jana na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji BBC, Mbowe alisema wao kama Chama wamekuwa na utaratibu wa kutoa msimamo wao na kueleza kuwa kwa siku za hivi karibuni wamekuwa na malalamiko dhidi ya Rais na Serikali yake kuhusu kuminywa kwa Uhuru wa Bunge, Mahakama na kuminya Demokrasia.

" Tunaona jinsi ambavyo uhuru wa watu unaminywa, uhuru wa vyombo vya habari, wandishi, wanasiasa na wananchi kutekwa, kudorora kwa uchumi, unaanzaje kumuunga mkono Rais nafikiri muhusika aulizwe mwenyewe," alisema Mbowe.

Kuhusu kauli ya Lowassa kusifia ongezeko la ajira, Mbowe anasema hayupo tayari kujibu hoja hiyo lakini akaeleza namna ambavyo makampuni mengi yanafungwa hivi sasa, kundi kubwa la vijana wasio na ajira likiwa mitaani.

" Nisikitike tu kuwa sisi tuna tatizo kubwa sana la kumuuguza Lissu ambaye alipigwa na risasi, kweli anaweza kutoka kiongozi mkubwa na kumsifia Magufuli wakati tunauguza watu? 

"Msaidizi wangu Ben Saanane amepotea hadi leo, wabunge wetu wanafukuzwa bungeni hivyo niseme tu hakuna msimamo kama huo ndani ya Chama labda atafutwe muhusika mwenyewe aeleze," Alisema Mbowe.

Akizungumzia hama hama kwa wabunge na wanachama wa upinzani na kujiunga na CCM sambamba na tukio la jana  la Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama hicho, Muslim Hassanal kujiunga na CCM , Mbowe alisema suala la wapinzani kuhamia CCM halijaanza leo na kwamba suala la kujenga upinzani ulio imara lazima lipitie hatua mbalimbali ili kufanya mchujo wa kubakia na watu wenye dhamira ya kweli.