SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 3 Desemba 2017

T media news

Polisi na TCRA wazungumzia kilichoitokea akaunti ya Mange Kimambi

Jeshi la Polisi limetaka liachwe liendelee kufanya kazi yake kwa weledi katika kushughulikia suala la Mtanzania aishiye ughaibuni, Mange Kimambi, ambaye anatuhumiwa kuchapisha taarifa za kuwatusi mitandaoni watu mbalimbali, wakiwamo viongozi.

Pia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kuwashughulikia kisheria watu wanaodaiwa kutumia mitandao vibaya, akiwamo Kimambi na kwamba hawahusiki na lolote kuhusiana na akaunti za mtuhumiwa huyo.

Polisi na TCRA walitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa kwa nyakati tofauti kama vyombo hivyo vinahusika kwa namna yoyote na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii jana kuwa akaunti ya Kimambi imefungiwa rasmi, ingawa taarifa nyingine zilimkariri Mtanzania huyo aishiye Marekani kuwa kilichotokea ni matokeo ya kazi ya wadukuzi wa mitandaoni, maarufu kama ‘hackers’.

Akizungumza kuhusiana na uwezekano wa wao kuifunga akaunti ya Kimambi ikiwa sehemu ya hatua wanazochukua kwa sasa, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa, alisema ni kweli jeshi lao linalifanyia kazi suala hilo.

Hata hivyo, hakutaka kukubali au kukataa juu ya kile kilichodaiwa kutokea kwenye akaunti ya Kimambi na badala yake kutaka apewe muda wa kulifanyia kazi ndipo alitolee maelezo ya kina.

“Hili jambo lina mambo mengi sana. Watu wengi wanahusika na taasisi nyingi (pia) zitahusika kulishughulikia,” alisema Mwakalukwa na kuongeza:

“Hivyo tunaendelea kupokea mawazo ya watu mbalimbali kuhusu namna ya kwenda nalo… mawazo wanayotupa tunayafanyia kazi lakini naomba mtuache kwanza tunaendelea kulishughulikia,” alisema Mwakalukwa.

Wakati msemaji wa Polisi akisema hayo, TCRA ilisema kuwa haiwezi kufunga wala kuingilia akaunti ya Kimambi kwa sababu huo siyo wajibu wake kisheria.

Msemaji wa TCRA, Semu Mwakyanjala, alieleza kuwa mamlaka yao haina nguvu za kisheria kufanya kazi hiyo bali wenye wajibu wa kufanya hivyo ni kitengo cha kudhibiti uhalifu wa mitandaoni cha Jeshi la Polisi.

Akifafanua zaidi, msemaji huyo alisema makosa yote yanayohusu mitandao, yakiwamo ya watu kutishiwa maisha, kutukanwa, kuibiwa kwa njia ya mtandao au kunyanyaswa kwa namna yoyote mtandaoni, wanaohusika ni polisi na siyo TCRA.

“Masuala ya akaunti za watu kwenye mitandao kama hiyo unayosema (ya Kimambi)… mwenye mamlaka ya kuingia na kuzifunga ni Jeshi la Polisi. Bunge liliipa mamlaka ya kisheria polisi kuchunguza na kukamata wahalifu kama hao… waulizeni wao,” alisema Mwakyanjala.

Kilichotokea Jana, Kimambi ambaye huchapisha masuala mengi yenye utata yakiwamo yahusuyo siasa za nchini, alionekana kana kwamba (kama ni yeye) amechapisha taarifa akilalamika kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna watu wameishikilia akaunti yake kwa kuwa alikuwa anakaribia kulipua bomu.

Aidha, katika akaunti inayofahamika kuwa ni Kimambi, ujumbe wa lugha ya kigeni ulionyesha kuwa akaunti hiyo imefungwa na waendeshaji wa mtandao wa Instagram kwa sababu ya kuwapo kwa malalamiko dhidi ya machapisho ya akaunti hiyo.

Pia upo ujumbe ulioonyesha kuwa ni wa Kimambi ukieleza kuwa ameamua kujiondoa mitandaoni baada ya kutafakari sana na hivyo kuifunga akaunti yake yenye wafuasi takribani milioni mbili.

“Nimetafakari sana juu ya nchi yangu ninayopoteza muda kuipigania, nimetafakari sana juu ya watu ninaowapigania, nimehatarisha maisha yangu na familia yangu, lakini naona napoteza muda wangu bila sababu za msingi. Nimeamua kufuta akaunti yangu Instagram na kuachana kabisa na masuala ya mitandao. Kwaherini Watanzania tutaonana duniani au mbinguni,” ulisomeka ujumbe mmojawapo ambao awali ulionekana kuwa ni wa Kimambi kabla taarifa nyingine kudai kuwa ni ujumbe ‘uliopostiwa’ na wadukuzi.

HT @ NIPASHE