Bosi wa benchi la Ufundi la Azam FC, Mromania, Aristica Cioaba, amefunguka kuwa licha ya mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Mghana, Bernard Arthur kuanza kuonyesha uwezo mkubwa wa kufunga lakini ataitumia michuano ya Kombe la Mapinduzi kujua uwezo wake.
Arthur amejiunga na Azam katika usajili wa dirisha dogo kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Liberty Professional, amekuwa na mwenendo mzuri wa kufunga katika mechi mbili za kirafiki alizocheza.
Cioaba alisema kuwa atatumia michuano ya Mapinduzi katika kujua uwezo wa mchezaji huyo licha ya kuanza kuonyesha uwezo mkubwa katika safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa tatizo.
“Timu ipo vizuri, tunashukuru tumeweza kufanya vizuri katika huu mchezo na kila mchezaji ameonyesha utofauti katika kutafuta matokeo, haijalishi tumecheza na timu ya aina gani, kikubwa kilikuwa ni kuangalia timu yangu ipoje.
“Kuhusu Arthur, nadhani bado anahitaji muda zaidi, sawa leo (juzi) ameweza kufunga mabao kwa uhakika kitu ambacho mwanzoni kilikuwa tatizo katika timu yangu kutokana na wachezaji ambao walikuwepo, zaidi nitaitumia Kombe la Mapinduzi kujua uwezo wake halisi kwa sababu hatutaweza kuwa na Mbaraka Yusuf kwa kuwa ni majeruhi," alisema Cioaba.