BAADA ya kufanikiwa kuifungia bao la ushindi timu yake dhidi ya Mbeya City, kiungo wa Simba, Shiza Kichuya amesema kuwa sasa ameanza kazi ya kuhakikisha anaendeleza kasi ya kufumania nyavu.
Kichuya amefikisha mabao matano sawa na Ibrahim Ajibu wa Yanga huku mshambuliaji Emmanuel Okwi akiongoza kwa kuwa na mabao nane.
Aidha, kiungo huyo msimu uliopita alimaliza ligi kwa kufunga mabao 12 sawa na Obrey Chirwa na Amissi Tambwe wa Yanga, Mbaraka Yusuph aliyekuwa Kagera Sugar msimu uliopita sasa Azam FC.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kichuya alisema kuwa kazi yake ni kufunga na anajipanga kuona anaendeleza kasi ya kufumania nyavu katika kila mechi.
“Nimejipanga kuhakikisha nafanikiwa kuifungia timu yangu katika kila mechi pale ninapopata nafasi ya kufanya hivyo kwani kila mechi ambayo tunacheza inakuwa na ugumu wa hali ya juu, hivyo tunapambana.
“Nafunga kwa ajili ya kuisaidia timu yangu iweze kufanya vizuri na kusonga mbele katika msimamo wa ligi kwa kupeana ushirikiano ipasavyo na wachezaji wenzangu.
“ Kwa upande wangu sifungi kwa ajili ya kushindana na mtu, bali ninachokifanya ni kwa ajili ya kutoa mchango wangu katika timu tu mabao nitakayomaliza nayo kwenye ligi ndiyo hayo Mungu atakayonijaalia kufunga lakini kasi yangu ya kupambana sasa inaongezeka,” alisema Kichuya.