Baada ya kuvuja kwa picha za staa wa filamu Bongo, Irene Uwoya (pichani) akiwa na staa wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ kuonesha wamefunga ndoa kisha mumewe Hamad Ndikumana ‘Katauti’ kuanika kifaa chake kipya, padri wa kanisa moja lililopo jijini Dar, ameibuka na kuwalipua wanandoa hao kwa kuishi kinyume na matakwa ya Kikristo.
ISHU ILIVYOANZA…
Hivi karibuni habari ya mjini kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na mitaani gumzo ilikuwa ni Uwoya kafunga ndoa na Dogo Janja lakini baadaye ilibainika kwamba ilikuwa ni kiki kwani walikuwa wanashuti video ya muziki.
NDIKUMANA AJIBU
Kutokana na hali hiyo Ndikumana au Ndiku naye aliamua kujibu mapigo ambapo aliweka picha kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa kimahaba na mrembo mmoja ambaye alitambulika kwa jina la Asma anayedaiwa kuwa ni Mrundi mwenziye.
Ili kuonyesha kwamba amedhamiria, Ndikumana alisindikizia picha hizo na maneno ‘sina habari na mtu nadeka zangu’. Baadaye akaongeza: ‘kata mti, panda mti.’
Baadhi ya mashabiki walionekana kumuuliza kwamba anamjibu Uwoya baada ya kusemekana ameolewa ambapo aliwajibu: ‘aolewe, asiolewe mimi nina msimamo wangu na maisha yangu muda mrefu sana, mnataka kunipangia? Sijali mnayofikiria kwa sababu binadamu siku zote ndiyo tulivyo, mimi ninafanya kinachouridhisha moyo wangu’.
NDUGU WA MWANAMKE WAJA JUU
Hata hivyo, baada ya kuanika picha hizo akiwa kimahaba na mwanamke huyo, tetesi zinadai kwamba ndugu zake mwanamke walikuja juu kwamba ni kwa nini ameamua kupiga picha na mwanaume huyo na kuziachia.
“Yaani unaambiwa ndugu wa Asma walikuja juu sana baada ya Ndikumana kuachia picha hizo mitandaoni, hali si shwari kabisa katika familia yao huku Burundi,” kilisema chanzo.
AMANI LATHIBITISHA FAMILIA KUTIBUKA
Amani liliingia mzigoni na kufanikiwa kuzungumza na mmoja wa marafiki wa Asma aliyeko jijini Dar ambaye alithibitisha kuwa mrembo huyo amecharukiwa vibaya na wazazi wake baada ya kuona picha hizo za kimahaba zilizopostiwa na Ndikumana.
TUJIUNGE NA PADRI SASA…
Akizungumzia suala hilo kiimani, padri wa kanisa moja jijini Dar ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini, alisema, kitendo anachokifanya Uwoya na Ndikumana hakileti picha nzuri kwani ndoa ya Kikristo ambayo imefungwa kanisani, haivunjiki kirahisi.
KANISA LINAITAMBUA NDOA
Aliendelea kusema kuwa, hata kama wawili hao walitengana na kila mmoja kuwa na maisha yake siyo kwamba ndiyo ndoa imevunjika bali wao kanisa linawatambua kama wanandoa, hivyo vitendo vyao vya kujiachia hovyo na wanawake au na wanaume ni kinyume kabisa na imani ya kanisa.
“Huyo Uwoya nimekuwa nikisoma kwenye mitandao ya kijamii mara utasikia yupo na mwanaume huyu mara kabadilisha, kwa kweli dini hairuhusu mambo hayo.
“Ndoa yao ipo hai kanisani kwa sababu kwa dini yetu hakuna talaka, labda itokee kuna tatizo kubwa kama utagundua kwamba mmojawapo anazini na ushahidi ukawepo au ana tatizo la kinyumba ambalo halitatuliki ndiyo ndoa inaweza kubatilishwa lakini kimsingi kanisa halitambui talaka.
“Kanisa linakataza kabisa uzinzi. Wanachokifanya kwa sasa ni zinaa. Kitendo hicho hakimpendezi Mungu kwa kuwa ni kinyume na imani na Biblia inavyosema, wanatakiwa wabadilike na wakae pamoja wamalize tofauti zao,” alisema padri huyo.
TUJIKUMBUSHE
Uwoya na Ndikumana walifunga ndoa mwaka 2009 katika Kanisa Katoliki, Mt. Joseph jijini Dar lakini walitengana na mpaka sasa Ndikumana bado hajatoa talaka rasmi kwa kile alichodai kuwa yupo kwenye harakati za kushughulikia mahakamani kwani ameshamtuma mtu jijini Dar.