SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 5 Novemba 2017

T media news

Samatta Acheza Mechi ya 70 Akiwa na KRC Genk

NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amecheza mechi yake ya 70 KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena, Genk.

Samatta alicheza kwa dakika 40 tu kwenye mchezo wa jana, kabla ya kumpisha Nikolaos Karelis aliyekuwa anacheza kwa mara ya pili tangu arejee uwanjani baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.

Katika mechi hizo 70, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mechi za mashindano yote tangu alipowasili Genk Januari mwaka jana akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika mechi hizo, Samatta ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika mwaka jana alipokuwa na Mazembe, 41 ameanza na mechi 24 ametokea benchi.

Na baada ya mchezo huo, Samatta aliyetajwa katika orodha ya wachezaji 30 ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wanaowania tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika, anarejea nyumbani kujiunga na timu yake ya taifa kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Benin wiki ijayo.

Baada ya kucheza nyumbani mfululizo mechi za kirafiki za kimataifa, Taifa Stars sasa itatoka mwezi huu kwenda Benin kucheza na wenyeji Novemba 11, mwaka huu na kikosi cha wachezaji 24 kitaingia kambini leo  mjini Dar es Salaam kabla ya kusafiri Novemba 9 kwenda Benin tayari kwa mchezo huo.

Kikosi cha KRC Genk kilikuwa: Vukovic, Uronen, Colley, Aidoo, Mata/Maehle dk84, Heynen, Malinovskyi, Pozuelo, Writers/Benson dk79, Samatta/Karelis dk40 na Ingvartsen.

Sporting Lokeren : Verhulst, Maric, Skulason, De Sutter/Enoh dk74, Kehli/Söder dk90, Ticinovic/Marzo dk79, Rassoul, De Ridder, Filipovic na Mpati.