Moshi. Kaimu Katibu mkuu wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka, amevitaka vyombo vya usalama kuwashughulikia wanasiasa wanaohubiri udini na ukabila.
Shaka ameyasema hayo leo Novemba 4 wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kata ya Bomambuzi katika Manispaa ya Moshi, na kusisitiza kuwa vipo vyama vya siasa ambavyo vinataka kuwagawa watanzania.
“Tunu kubwa ya taifa letu ni upendo na amani kwa hiyo vyombo vya ulinzi na usalama viwashughulikie wanaohubiri udini, ukabila na ukanda ili kujipatia umaarufu wa kisiasa,” amesema.
Shaka aliwaambia wananchi waliofurika katika mkutano huo uliofanyika viwanja vya soko la Pasua kuwa, alisema pamoja na yote yaliyojitokeza katika mkoa huo, bado wana imani na CCM.
Katika mkoa wa Kilimanjaro, upinzani unashikilia majimbo saba kati ya tisa huku CCM kikishikilia majimbo mawili tu ya Mwanga na Same Mashariki huku upinzani pia ukishikilia Halmashauri tano.
“Pamoja na yote yaliyojitokeza katika mkoa Kilimanjaro na kata mbalimbali bado mmeonyesha imani kubwa kwa Serikali ya CCM. Nawasihi sana katika uchaguzi huu msifanye makosa,” amesisitiza.
Pia ametumia mkutano huo kuwasihi wana CCM kutowabagua wala kuwatenga wanaorudi CCM wakitokea upinzani ambapo katika mkutano huo, baadhi ya wafuasi wa Chadema walijiunga na CCM.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM mkoa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya, amewaomba wananchi kumchagua mgombea Udiwani wa CCM, Juma Raibu akisema amejipanga vyema kuwatumikia.
Katika mkutano huo, aliyekuwa mmoja wa marafiki wa Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Fred Mushi, alipewa fursa ya kuhutubia, na kusema huko upinzani alikoenda alikutana na moto.
Mushi ambaye alikuwa mwenyekiti wa UVCCM mkoa Kilimanjaro kati ya 2012 hadi 2015 alipojiuzulu na kumfuata Lowassa, alirejea tena CCM wiki mbili zilizopita akisema anamuunga mkono Rais John Magufuli.
Mwananchi: