Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala amemlipua waziri wa zamani wa wizara hiyo, Lazaro Nyalandu akimtuhumu kwa matumizi mabaya ya madaraka na kumlalamikia kupoteza mabilioni ya fedha za Serikali.
Akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 207/2018, Bungeni Jijini Dodoma, Dk Kigwangalla ameiagiza Takukuru na polisi kumchunguza Nyalandu.
Dk Kigwangala amesema Nyalandu aliikosesha Serikali mapato ya Sh32 bilioni kwa miaka miwili aliyohudumu katika wizara hiyo kwa kushindwa kusaini sheria ya tozo kwa hoteli za kitalii.
Mbali na tuhuma hiyo, pia alimtuhumu kutumia helkopta ya mwekezaji mmoja raia wa kigeni, kipindi cha kampeni zake za kugombea urais 2015, wakati kampuni ya raia huyo ilikuwa ikituhumiwa kwa ujangili.
Hata hivyo wakati Kigwangala akitoa tuhuma hizo tayari Nyalandu alishasema kuwa tuhuma ambazo zimeanza kuibuliwa mitandao dhidi yake si za kweli bali zinalenga tu kumchafua.
Taarifa hiyo imekuja kipindi ambacho Lazaro Nyalandu amejiondoa CCM na kujiunga CHADEMA.