Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Respicious Mwijage ameuambia upande wa mashtaka kuwa siku akipandwa na mashetani ataifuta kesi ya vigogo wa Mamlaka ya Vitambulisho vyaTaifa (NIDA) endapo kama upelelezi hautakamilika.
Hakimu Mwijage alitoa angalizo hilo baada ya Wakili wa Serikali, Peter Vitalis kueleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na baada ya kusema hayo, Hakimu Mwijage alisema kesi hiyo ina takribani siku 365 na upelelezi haujakamilika jambo ambalo linatoa taswira mbaya.
“Kamilisheni upelelezi ili kama hawa wamekula fedha za umma wafungwe au kama hawajala waachiwe huru, siku mashetani yangu yakipanda nitafuta hii kesi.”
Hakimu Mwijage aliahirisha kesi hiyo hadi December 6,2017 huku akiutaka upande wa mashtaka kufika na taarifa kuhusu upelelezi.
Kesi hiyo inamkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake saba, ambao wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.16.
Mbali na Maimu, washtakiwa wengine ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Xavery Kayombo, Meneja Biashara wa mamlaka hiyo, Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph Makani.
Washtakiwa pamoja na mashtaka mengine yakiwemo kuisababishia Serikali hasara wanadaiwa tarehe tofauti kati ya January 15 hadi 19, mwaka 2010 katika Makao Makuu ya NIDA wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo bila kufuata viwango vya kubadilishia fedha.