Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kimesema kwamba, sababu zilizotolewa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu za kujiuzulu ubunge na uanachama wa chama hicho hazina mashiko, isipokuwa kilichomsukuma kufukia uamuzi huo ni hasira za kukosa uwaziri katika serikali ya awamu ya tano.
Hayo yalisemwa na Katibu wa CCM Mkoa Singida, Jamson Mhagama na kusisitiza kuwa asitegemee tena kushinda kiti cha ubunge kupitia CHADEMA anakolilia kwenda sababu CCM itashinda mchana kweupe.
Aidha, Mhagama alisema kwamba chama hicho kinamtakia kila la kheri huko na anakokwenda na kwamba katika uchaguzi mdogo wa ubunge utakaofanyika kujaza nafasi hiyo, watashinda kwa kishindo.
“Tunamtakia kila la kheri. Ila tunamwonya kuwa asitarajie tena kupata ubunge kupitia CHADEMA anakolilia kwenda, CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mdogo ujao.”
Baadhi ya wakazi wa jimbo la Singida Kaskazini waliotoa maoni kuhusu kujiuzulu kwa mbunge wao, walisema kila mwananchi ana haki ya kuchagua chama anachotaka, lakini akasema kabla mbunge wao huyo waliyemchagua hajazungumza na watanzania kuhusu kujiuzulu kwake, angewaambia kwanza wapigakura wake waliomchagua.
Wakazi wengine walikerwa na uamuzi wa Nyalandu kutangaza kujiuzulu ubunge akiwa Arusha wakidai kwamba hiyo ni ishara ya kutokuwaheshimu kwani alitakiwa atangazie uamuzi huo kwa wananchi waliomchagua.
Nyalandu kwa upande wake, amewashukuru watu wote waliomtumia salaamu na kuunga mkono kwa hatua niliyochukua huku akiwataka watanzania waunganie kwani hoja zilizombele yao ni kubwa na zenye kuhitaji mshikamano.