Na Mathias Canal, Arusha
Serikali imekuwa ikiongeza idadi ya wanafunzi katika Vyuo vya Kilimo na kwa sababu hiyo Maafisa Ugani wamekuwa wakiongezeka kila mwaka ambapo hali hiyo imewezesha Karibu kila Kata hapa nchini kuwa na Afisa Ugani.
Lakini pamoja na kuwepo kwa wataalamu hao wa kilimo bado uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini yakiwemo mazao ya chakula na biashara si wa kuridhisha ambapo wakulima wanalima na kupanda pasina hata kufuata hatua za kitaalamu.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Mhandisi Methew John Mtigumwe wakati wa kikao cha kazi akizungumza na wakufunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mboga Matunda na Maua (HORTI TENGERU) kilichopo katika Kijiji cha Tengeru, Kata Patandi, Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha.
Alisema lengo la Serikali kusambaza Maafisa Ugani kwenye Halmashauri mbali mbali nchini ilikuwa kuwasaidia wakulima waweze kufanya Kilimo kwa Ufanisi na kuongeza mavuno.
Hata hivyo jambo hilo limekuwa kinyume kwani asilimia kubwa ya maafisa ugani ama hawafanyi kazi zao ipasavyo ama wameshindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo.
Mhandisi Mtigumwe alisema kuwa Wizara ya kilimo inaandaa utaratibu wa kuwarudisha shule maafisa ugani wasiofaa kutokana na uchache wa ellimu zao na uwajibikaji huku wale ambao watashindwa kabisa kuwa msaada kwa wakulima baada ya masomo wizara itapendekeza waondolewe kazini.
Alisema Maafisa ugani hao Watafanyiwa usaili upya ili kubaini uwezo wao kwani wengi wao wameajiriwa na serikali lakini wakulima hawanufaiki na kilimo tafsiri yake Wataalamu hao ama hawatekelezi wajibu wao au hawana uwezo wa kutekeleza ipasavyo.
Aidha, alisema Maafisa ugani kote nchini wanatakiwa kuwekeza kwenye utoaji wa Huduma ya Ugani kwa Wakulima ili iwe rahisi kwa Mkulima kusaidika katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya biashara na kilimo.
Sambamba na hayo pia aliwasihi Wakufunzi katika chuo hicho kujiendeleza kielimu huku akisema kuwa Wizara ya kilimo lazima itengeneze mpango wa kuwaendeleza wakufunzi ili kuzalisha wataalamu wenye ufanisi zaidi.
Alisema anatambua kuwa Mahitaji ni makubwa katika vyuo vya kilimo hivyo Wizara inatazama namna ya kuongeza chuo kingine kama hicho huku akiwasisitiza wataalamu hao kubadili mfumo badala ya kusoma kwa jumla masomo mengi na kufikia hatua ya kuchagua eneo maalumu la kusoma (Kozi) kwani Kilimo ni somo pana.
“Nategemea muandae mpango maalumu ambao utapelekea Kuwa na kozi za muda mchache sio lazima kuwa na kozi za muda mrefu pekee kama ilivyo hivi sasa” Alisema Mhandisi Mtigumwe
Katika hatua nyingine amewataka Watumishi wote kuongeza spidi katika utendaji wa kazi ili kuunga mkono juhudi za Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na serikali ya awamu ya tano yenye kauli mbiu ya HapaKaziTu.
Sambamba na kutembelea na kuzungumza na watumishi na wakufunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mbogamatunda na Maua (HORTI TENGERU) Akiwa ziarani Mkoani Arusha Katibu Mkuu Mhandisi Methew Mtigumwe alitembelea pia Taasisi ya Utafiti Horti Tengeru, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Maendeleo Kanda ya Kaskazini (NZARDI) na Taasisi ya Utafiti ya kudhibiti visumbufu katika Ukanda wa Tropiki.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Mhandisi Methew John Mtigumwe akizungumza wakati wa kikao cha kazi na watumishi wa Taasisi ya Horti Tengeru na wakufunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mboga Matunda na Maua (Horti Tengeru).
Baadhi ya watumishi wa Taasisi ya Horti Tengeru na wakufunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mboga Matunda na Maua (Horti Tengeru) wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Mhandisi Methew John Mtigumwe wakati wa kikao cha kazi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Mhandisi Methew John Mtigumwe akiwasili katika Ofisi za Taasisi ya Horti Tengeru na Chuo cha Mafunzo ya Mboga Matunda na Maua (Horti Tengeru). Mwingine ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utafiti Dkt Mansoor Hussein.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Mhandisi Methew John Mtigumwe akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Taasisi ya Horti Tengeru na Chuo cha Mafunzo ya Mboga Matunda na Maua (Horti Tengeru).
Baadhi ya watumishi wa Taasisi ya Horti Tengeru na wakufunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mboga Matunda na Maua (Horti Tengeru) wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Mhandisi Methew John Mtigumwe wakati wa kikao cha kazi.
Afisa Mfawidhi -Horti-Tengeru akisoma Risala kwa niaba ya watumishi wenzanke wakati wa kikao cha pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Mhandisi Methew John Mtigumwe wakati wa kikao cha kazi.
Baadhi ya watumishi wa Taasisi ya Horti Tengeru na wakufunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mboga Matunda na Maua (Horti Tengeru) wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Mhandisi Methew John Mtigumwe wakati wa kikao cha kazi.