SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 17 Oktoba 2017

T media news

Zitto Kabwe athibitisha kupokea barua ya kujiuzuru Mwigamba

Chama cha ACT- Wazalendo kitakutana Ijumaa Oktoba 20, 2017 kujadili masuala kadhaa, likiwemo la kujizulu kwa mwenyekiti wake wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Samson Mwigamba.

Mwigamba leo Jumatatu, Oktoba 16 ameandika barua ya kujizulu uongozi na kueleza atabaki kuwa mwanachama wa kawaida ili aweze kupata fursa ya kuwahoji kwa matendo viongozi.

"Nimeamua kukaa kando kwa kuwa tumekuwa hatukubaliani na baadhi ya mambo ndani ya chama na hasa kiongozi wetu… wacha nikae pembeni niwe mwanachama ili niwe na nafasi ya kuwahoji vizuri viongozi wetu masuala mbalimbali na nitabaki kuwa mwanachama mwema,’’ amesema alipozungumza na Mwananchi.

Akizungumzia uamuzi huo, Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe amesema, “Nimepokea barua yake. Tutatafakari suala hilo na masuala mengine yanayohusiana na hayo kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi wa chama Ijumaa.”

“Ndugu Mwigamba ataalikwa kwenye kikao hicho. Ninamshukuru sana kwa utumishi wake uliotukuka kwenye chama na ninamtakia kila la kheri. Mchango wake na kujitoa kwake kwa hali na mali hakutasahaulika kwenye chama chetu,” amesema  Zitto.