Ungetegemea kuona watu wanaokwenda Nairobi kumjulia hali mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu wakirudi na amani kwamba wamekuta anaendelea vizuri, lakini ni tofauti; wanaonekana jasiri zaidi na tayari kwa mapambano.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Mchungaji Peter Msigwa, Zitto Kabwe, Lazaro Nyalandu, Julius Mtatiro na Sheikh Ponda Issa Ponda waliporejea kutoka jijini humo kumjulia hali mwanasheria huyo mkuu wa Chadema.
Lissu, ambaye amelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari lake nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma.
Alihamishiwa Nairobi usiku wa siku ya shambulio hilo linaloonekana lililenga kuchukua maisha yake, na kwa mujibu wa wanaokwenda kumjulia hali, afya yake inazidi kuimarika.
Lakini, jambo moja ambalo limeonekana kwa wengi waliomjulia hali ni kauli zao baada ya kurejea; wanaonekana sasa hawaogopi kifo, wako tayari kupambana na yeyote wanayedhani ni adui, wameongezeka ujasiri na si waoga katika kuzungumza.
Wengi wao waliporudi walizungumza kwa ujasiri zaidi na hata walipozungumza na Mwananchi walionekana kusimamia kauli zao.
“Ukizungumza na Lissu, usipopata ujasiri basi unapaswa ujiulize mara mbili juu ya uwepo wako katika siasa,” anasema Mchungaji Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chadema.
Msigwa anasema alivyokutana na hali ya Lissu na maneno ya kishujaa aliyozungumza, yamezidi kumtia ujasiri wa kusonga mbele katika kudai haki.
Ameona hakuna cha kupoteza
Alisema ujasiri huo umeongezeka kutokana na kuona hakuna cha kupoteza.
“(Ukizungumza na Lissu unapaswa ujiulize) Juu ya unachofanya kuhakikisha haki inapatikana, juu ya nafasi yako katika kutetea haki ya Watanzania na demokrasia kwa ujumla,|” anasema.
“Maana yake nini? Maana yake ni kwamba tunatakiwa kufika mbali zaidi ya alipofika yeye. Nani muoga tena leo.”
“Tuna imani tukifa leo, wapo watakaohoji kifo chetu, huku waliotuua nao watakufa kama si leo kesho baada ya kutekeleza mauaji yetu, kila mmoja atakufa haijalishi kwa kifo cha aina gani, Lissu anatoa mwanga wengine tunaufuata. ”
Msigwa alitumia msemo wa “kama huna cha kukifia, huna sababu ya kuishi”, kwa hiyo wamepata kitu cha kufia.
Maneno kama hayo yamesemwa na Zitto, ambaye ni kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na mbunge wa Kigoma Mjini.
Zitto na maneno mazito
Zitto anajulikana kwa mapambano ya hoja na siasa za kistaarabu, lakini katika siku za karibuni ameonekana kutoa maneno mazito yaliyomfanya aingie matatani na vyombo vya dola.
“Siku mbili hizi nilizoenda kumuona Lissu zimeniacha nikiwa na mawazo sana, nimerudi nchini nikiwa mwenye unyenyekevu zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri ambao ndugu yangu amenionyesha,” ameandika Zitto katika ukurasa wake wa Facebook.
“Siyo mara nyingi hapa nchini kusikia tukiongelea ujasiri, lakini namfikiria Lissu na vile nilivyojisikia nikiwa pamoja naye Nairobi, najua hivyo ndivyo alivyo.”
Zitto pia amezungumzia hali ya Lissu inavyowafanya watu waongeze ujasiri.
“Ukiona hali ya Lissu, unaumia sana. Kosa lake nini?” anahoji.
“Lengo la waliompiga ni nini? Kumnyamazisha kabisa? Jawabu kwa hao waliomshambulia Lissu ni nini? Kuwa kama Lissu. “Hawawezi kutuua wote. kama kila mmoja akiwa mkali kama Lissu, wauaji hawatafanikiwa kwani hawawezi kutuua wote.”
Amesema pia kuwa Lissu alimwambia kuwa waendelee alipoishia na akipona ataanzia walipofikia.
“Hivyo ninamshikia ninamshikia Lissu zamu na naomba kila mwenye uwezo afanye hivyo ili kulinda uhuru wa kukosoa na uhuru wa mawazo,” ameandika Zitto.
Kiongozi mwingine aliyepata fursa ya kumuona Lissu ni mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ambaye alisema kama kuna Mtanzania imara, asiyeogopa na mwenye maono makubwa ni Lissu.
‘Kawaambie nitarudi mzima’
Alisema risasi zote zilizopenya kwenye mwili wa Lissu, zimemtengenezea “uimara maradufu, mara sabini, mara mia moja”.
“Waliodhani kuwa kumuua Lissu ndiyo kuua harakati za Watanzania za kudai taifa la haki na linalofuata misingi ya sheria na katiba bora, wamejidanganya,” anasema Mtatiro.
“Lissu ameniambia ‘Mtatiro nenda kawaambie kuwa nitarudi nikiwa mzima na tutaendelea na mapambano maradufu zaidi, faraja muhimu ninayohitaji kutoka kwa Watanzania hivi sasa ni kuendeleza mapambano ya kudai haki.”
Mtatiro alisema alichojifunza kwa Lissu na kinachompa ujasiri ni kusema ukweli.
“Ukizungumza naye (Lissu) ni kama anakusuta jinsi alivyo jasiri. Anakusuta kwa maana yeye yupo tayari kufa au kupambania uhai wake ili aikomboe nchi kutokana na kila aina ya udhalimu,” alisema Mtatiro.
Mtatiro alisema ukimuona Lissu kitandani, unamuona mtu ambaye bado ana ari kubwa ya kuitetea nchi yake pamoja na yote yaliyomkuta.
Alisema hali hiyo inakufanya uwaze mara mbili una kipi cha kupoteza wewe ambaye hujafanywa kitu chochote.
Alisema hata mkewe ambaye ungetegemea umkute ametetereka, amechanganyikiwa au ana hofu, lakini anakupokea kwa bashasha na ujasiri wa wazi.
Lissu na marejeo ya sheria
Alisema ukizungumza na Lissu anatumia muda mwingi kukupitisha kwenye vifungu vya sheria, michakato ya kudai haki katika mataifa mengine na kukusisitiza kuwa imara kuendelea kulipigania taifa kwa njia za kidemokrasia.
“Ukienda kumuona Lissu uzalendo wako, usimamizi wako wa demokrasia katika nchi kama ulikuwa na mashaka, ukizungumza naye unajengeka na unapata ujasiri zaidi,” alisema.
Alisema kupona kwa Lissu kumeongeza hamasa hata miongoni mwa wananchi ambao kwa vitendo wameonyesha nia ya kutaka kwa kila hali apone.
“Hii inaonyesha ni kwa namna gani wanaukubali mchango wake, sembuse mwanasiasa na kiongozi kama mimi. Hili limeniongezea kitu maishani,” alisema.
Pengine kauli za kijasiri zaidi ni zile zilizotolewa na Sheikh Ponda, ambaye ni katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, ambaye hadi jana alikuwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano baada ya kuzungumza na waandishi kuhusu safari yake ya Nairobi.
Alisema alikwenda Nairobi kwa lengo la kumfariji na kumtia nguvu Lissu, lakini mbunge huyo ndiye aliyefanya kazi ya kumpa ujasiri na kumtia nguvu.
“Nimepata ujasiri. Badala ya mimi kumpa matumaini, yeye ndiye aliyenipa matumaini,” alisema Sheikh Ponda.
Alisema Lissu alimwambia kuwa atarudi hivi karibuni katika harakati zake na ataanzia alipoishia na kwamba amemuhimiza mshikamano.
Naye Nyalandu, ambaye ni mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) amekuwa akitoa kauli tofauti tangu atoke kumuona Lissu jijini Nairobi.
Tabasamu pana
Nyalandu amekuwa akiandika katika akaunti zake za mitandao ya kijamii kuhusu haja ya kuwasaka waliomshambulia Lissu.
Alisema Lissu alikuwa na tabasamu pana alipokuwa akizungumza naye licha ya kuumia.
Nyalandu ni miongoni mwa viongozi waliokwenda kumuoa Lissu siku za awali kabisa tangu alipopigwa risasi mjini Dodoma.
Naye mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche alisema amepata ujasiri zaidi kwa sababu anaamini hakuna jambo linaloonyesha uwoga uliokithiri kama mtu anapofikiria kuua ili amnyamazishe mzungumzaji.
Alisema kutokana na hilo hakuna cha kuogopa zaidi ya kuzungumza, kwa sababu inaonyesha anayetakiwa kusikia kinachozungumzwa amekisikia na kimemtisha ndiyo maana anaamua kuua.
“Haitakuwa na maana kuwa mpinzani halafu ukawa mnafiki kwa kupindisha ukweli. Kusema ukweli kumemgharimu Lissu,” alisema.
“Ili kulipa damu yake iliyomwagika, tuliobaki tunapaswa kusema ukweli.”