SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 15 Septemba 2017

T media news

Spika wa Bunge Hana Mamlaka Kumzuia Mbunge Kuzungumza Bungeni

Baadhi ya wasomi wameichambua kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kwamba anaweza kumfungia Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe asizungumze bungeni kwa muda uliobaki na wengi wamesema hana mamlaka hayo.

Juzi, Spika Ndugai alisema bungeni kwamba: “Nina uwezo wa kumpiga marufuku (Zitto) kuzungumza hadi miaka yote mitano iishe hauna pa kwenda, hakuna cha swali, nyongeza wala kuzungumza utanifanya nini?”

Kauli ambayo Zitto aliijibu kupitia ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa Twitter akisema, “Nimegundua Spika Ndugai ameibua mashtaka yangu ili kufunika ufuatiliaji wa wananchi kuhusu (Tundu) Lissu kupigwa risasi. Nimeamua sitawapa hilo.”

Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, alipigwa risasi 28 mpaka 32, Alhamisi iliyopita mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge. Spika alisema risasi tano ziliupata mwili wake.

Mzozo kati ya Spika Ndugai na Zitto ulianza hivi karibuni baada ya kiongozi huyo wa ACT–Wazalendo kudai kuwa Bunge limewekwa mfukoni na Serikali, wakati alipotoa maoni kuhusu ripoti mbili za kamati ya Bunge kuhusu biashara ya almasi na Tanzanite.

Kutokana na kauli hizo, Spika Ndugai aliagiza mbunge huyo ahojiwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku akimshtaki kwa wapigakura wake kuwa licha ya mbunge wao kuwapo nchini, hajafika bungeni kuwawakilisha na yeye (Spika), hana taarifa.

Maoni ya wadau
Walipoulizwa kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu kuhusu suala la kumzuia mbunge kuzungumza kwa muda wote, baadhi ya wasomi walisema kauli kama hiyo haikupaswa kutolewa na Spika kwa kuwa inakiuka Katiba na kanuni za Bunge hilo. Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema kauli ya Spika Ndugai imelenga kuwanyamazisha wabunge wasiwe huru kutoa maoni yao kwa mujibu wa Katiba.

“Unless (labda) kama alikuwa anatania, lakini Spika hana mamlaka ya kumzuia mtu kuzungumza kwa kipindi chote hicho. Ni jitihada za kuwanyamazisha wabunge,” alisema Dk Kyauke.

“Kwa mfano, angalieni Bunge la Afrika Kusini jinsi Julius Malema anavyomkosoa Rais Jacob Zuma au Bunge la Kenya. Bunge kama chombo cha wananchi kinapaswa kuwa na nguvu ya kuisimamia Serikali kwa sababu kinatumia fedha za wananchi. Spika anaweza kukosolewa anapokosea, asiwatishe wabunge,” aliongeza Dk Kyauke.

Kuhusu kanuni za Bunge, Dk Kyauke alisema kosa la Zitto halihusiani na kanuni hizo kwa sababu mbunge huyo ametoa maoni yake akiwa nje ya Bunge na yuko huru kwa mujibu wa Katiba.

“Kwanza kanuni hazimpi mamlaka Spika kumzuia kuongea, lakini Zitto alitoa maoni yake nje ya Bunge,” alisema Dk Kyauke.

Kauli ya Dk Kyauke iliungwa mkono na Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba, Hebron Mwakagenda aliyesema hakuna kanuni inayomruhusu Spika kumzuia mbunge kuongea milele. “Kwanza hakuna kanuni ya Bunge inayomruhusu Spika kumzuia mbunge kuongea. Halafu anasema Zitto hawezi kwenda popote. Anaweza kwenda kushtaki mahakamani kama ataona hatendewi haki,” alisema Mwakagenda na kuongeza:

“Spika anapaswa kuonyesha uongozi. Kama Zitto amekosea, ampeleke kwenye Kamati ya Maadili, si kutoa kauli hizo ambazo zitatafsiriwa kuwa anaipa maelekezo kamati hiyo, vinginevyo tunaona anatekeleza maagizo ya Rais John Magufuli kwamba awashughulikie wapinzani bungeni na yeye atawashughulikia nje ya Bunge,” alisema.

Mwakagenda alimtaka Spika kuiona nafasi yake kama dhamana aliyopewa na Watanzania na wakiamua wanaweza kumwondoa kwa mujibu wa Katiba.

Alihoji pia sababu za Spika kuwaandama wabunge wa upinzani pekee ilhali wabunge wote wanafanya makosa.

“Ndugai anapoteza muda kwa kuhamisha ugomvi wake binafsi na mbunge mmojammoja na kufanya kuwa wa Bunge zima. Kwa nini iwe kwa wabunge wa upinzani peke yake? Mbona wabunge wa CCM wanaofanya makosa tunawaona?

“Cheo ni dhamana, wananchi wamempa Ndugai kwa miaka mitano tu. Kanuni zinawaruhusu wabunge kumwondoa Spika anapokosea,” alisema Mwakagenda.

Wakati Mwakagenda akisema hayo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema mkuu huyo wa mhimili wa Bunge hakupaswa kusema maneno hayo.

“Kwa mujibu wa Katiba na vigezo vya uongozi, Spika hakupaswa kutoa maneno yale. Kwa sababu yeye ni baba wa Bunge, wabunge wote wanamwangalia. Sasa anapotoa kauli hizo kwa wabunge inamshushia haiba yake. Inaonekana alipotoka,” alisema Mbunda.