SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 15 Septemba 2017

T media news

Spika Ndugai Awatahadharisha wabunge kuhusu Usalama Wao na Kutokaa Baa Muda Mrefu

Spika Ndugai leo amewausia wabunge wanzake kuwa makini na usalama wao kwa kuchukua hatua zaidi za kujilinda, ikiwemo kutokaa baa mpaka usiku wa manane ili kujiepusha na matatizo mbali mbali yatakayoathiri usalama wao. .

Akizungumza muda mfupi leo Ijumaa kabla ya kuahirishwa kwa Bunge, Ndugai aliwataka wabunge kutokaa sana katika mabaa.

“Yaani tuchukue hatua tu katika maisha yetu kama mnavyosikia matukio ni mengi katika nchi yetu. Ni vizuri usalama unaanza na wewe mwenyewe kwanza,”amesema.

Amesema vyombo vya usalama vinavyowalinda vinakuwa vinaongezea kidogo na kuwataka kutazama nyendo zao za namna ambavyo wanaishi.

“Kwa wale tuliozoea sana saa 7 ndio tunarudi nyumbani  basi tuanze kurudi mapema kidogo. Lakini pia tuangalie usalama wa familia zetu na tuwaambie wapigakura naona siku hizi watoto wanapotea, watoto wanauawa,”amesema.

Amewataka wabunge kuwapelekea huo ujumbe kuwa wawe makini na watoto wao wakati wa kwenda shule na maeneo mengine kwa kuhakikisha wanajua mtu anayewapeleka shule na kuwachukua.

“Hayo mambo yanayofanana na hayo. Ushauri ni wa ujumla tu,”amesema.

Aliwataka wabunge kuendelea kumuombea Tundu Lissu na wale watakaopata nafasi ya kwenda kumuona jijini Nairobi wampelekee ujumbe.

Amesema pia wabunge wawaombee wenzao ambao wamekwenda kumuuguza mbunge huyo lakini wanatukana kwa sababu hawajui watendalo.

Ushauri huo umekuja siku chache baada ya Lissu kujeruhiwa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.