SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 7 Septemba 2017

T media news

Rais Magufuli akutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula Duniani

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Bw. Jose Graziano da Silva amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Shirika hilo lipo tayari kushirikiana na Tanzania kufanya mageuzi katika kilimo kwa kuwezesha uzalishaji wa mazao na viwanda vya mazao hayo.

Bw. Jose Graziano da Silva amesema hayo jana tarehe 06 Septemba, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli na kumshukuru kwa ushirikiano mzuri ambao shirika hilo limeupata kwa kipindi cha miaka 40 ya uwepo wake hapa nchini.

Akitoa mfano wa nchi yake ya Brazil Bw. Jose Graziano da Silva amesema Tanzania inaweza kupata manufaa makubwa ya kuongeza uzalishaji wa chakula, kuuza nje ya nchi, kuzalisha ajira na kukuza pato la Taifa kupitia mapinduzi yatakayotokana na kuunganisha kilimo na viwanda vikiwemo vya kusindika nyama na samaki kwa kuwa fursa zipo nyingi.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Bw. Jose Graziano da Silva kwa kuja nchini na amemhakikishia kuwa Serikali itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano wake FAO, huku akitilia mkazo dhamira yake ya kutaka ushirikiano huo uelekezwe katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

“Tanzania ina maziwa mengi, ina ukanda wa bahari wenye urefu wa kilometa 1,422 na ina mito mingi ambayo inaweza kuwekezwa viwanda vya samaki, inashika nafasi ya pili kwa mifugo Barani Afrika, hivyo tunahitaji kujenga viwanda vya nyama.

“Asilimia 75 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana ambao wanauwezo wa kuzalisha mazao mengi ya kilimo tunahitaji viwanda, uchumi wetu ni mzuri na unakua kwa wastani wa asilimi 7.1 na mengine mengi, kwa haya yote tunahitaji wadau ikiwemo FAO tushirikiane kutumia fursa hizi” alisema Mhe. Rais Magufuli na kuahidi kuwa Serikali yake imejipanga kusimamia miradi yoyote itakayoletwa nchini ili itekelezwe kwa uadilifu na ubora wa hali ya juu.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mzee Joseph Butiku Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo Mzee Butiku amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuongoza Serikali ambapo katika kipindi kifupi amesimamia vizuri nidhamu, watu kufanya kazi, kupiga vita rushwa, ulipaji wa kodi na amemtaka asirudi nyuma kwa kuwa nchi inakwenda vizuri.

“Mimi nimefanya kazi hapa Ikulu kwa miaka 23, Mwl. Nyerere alijenga misingi mizuri, lakini huyu Rais Magufuli ameisimamia vizuri sana, unapofanya mambo kama haya, lazima hapa nyumbani na huko nje kutakuwa na maneno, mazuri sikiliza, ya hovyo achana nayo” alisisitiza Mzee Butiku.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli ameagana na Balozi wa China hapa nchini anayemaliza muda wake Mhe. Dkt. Lu Youqing na kumshukuru kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano aliyokuwepo hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli amesema katika kipindi chake Mhe. Dkt. Lu Youqing ametoa mchango mkubwa katika kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano kati China na Tanzania, uliofanikisha kuongeza uwekezaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu, elimu, kilimo, afya na kukuza biashara ambapo wafanyabiashara wengi wa China wamekuja kuwekeza nchini, mambo ambayo yamezalisha ajira na kukuza pato la nchi.

Mhe. Dkt. Magufuli amemuomba Mhe. Dkt. Lu Youqing kuendelea kuitangaza vyema Tanzania nchini China, ambako anakwenda kushughulikia masuala ya uchumi na kwamba anaamini atatumia nafasi hiyo kuhimiza wawekezaji na wafanyabiashara wengi zaidi wa China kuja kuwekeza hapa nchini.

“Mhe. Balozi Dkt. Lu Youqing Watanzania hatutakusahau kwa mchango wako, wewe ni ndugu na rafiki yetu, tunakushukuru sana kwa yote uliyoifanyia nchi yetu, naomba nikuhakikishie kuwa kazi nzuri uliyoifanya tutaiendeleza na tutashirikiana na Balozi mpya atakayekuja kuendeleza pale ulipoachia” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mhe. Dkt. Lu Youqing amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano alioupata kwa kipindi chote alichokuwepo hapa nchini na ameahidi kuwa ataendelea kuwa Balozi mzuri wa kuinadi Tanzania huko nchini China.

“Mhe. Rais Magufuli nakushukuru sana, hapa Tanzania ni nyumbani kwangu na nipo tayari wakati wote kutoa ushirikiano pale nitakapohitajika kufanya hivyo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini China ama kutoka Serikalini hapa Tanzania” Alisema Dkt. Lu Youqing.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam