Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametangaza kuwa hayuko tayari kushiriki marudio ya uchaguzi mkuu wa urais nchini humo.
Bwana Odinga amesema kuwa anataka kuwepo mikakati ya kisheria na kikatiba inayohitajika, kabla ya yeye kukubali kushiriki uchaguzi huo.
Bwana Odinga pia anataka mabadiliko kufanyiwa Tume ya uchaguzi nchini humo, ambayo imelaumiwa na mahakama ya juu kwa wa kuendesha uchaguzi kwa njia ambayo haiukuwa nzuri ambayo ilisababisha kufutiliwa mbali matokeo.
Jana Jumatatu Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini Kenya ilitangaza kwamba uchaguzi mpya wa urais nchini humo utafanyika tarehe 17 Oktoba.
Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema uchaguzi huo utashirikisha wagombea wawili pekee wa urais, Rais Uhuru Kenyatta na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.
"Hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wa urais katika uchaguzi huo upya. Waliopinga matokeo ya uchaguzi kortini, Bw Raila Odinga na mgombea mwenza wake Stephen Kalonzo Musyoka na mshtakiwa wa tatu Rais Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza wake William Samoei Ruto, watakuwa ndio wagombea pekee," taarifa ya bw Chebukati ilisema.
Katika kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, Mahakama ya Juu iliiwekea lawama Tume ya Uchaguzi.