SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 5 Septemba 2017

T media news

Mwili wa Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Handeni Muhingo Rweyemamu Waagwa

Waandishi wa habari wametakiwa kuyaishi aliyoyafanya mwandishi mkongwe na mkuu wa wilaya mstaafu, Muhingo Rweyemamu ikiwa ni ishara ya kumuenzi.

Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa mwanahabari huyo mjini hapa, kwa niaba ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Jesse Kwayu amesema hakuna cha zaidi cha kufanya kama wanahabari zaidi ya kutafakari aliyofanya Muhingo.

"Sisi TEF tuna msiba mkubwa si tu kwa kuondokewa na Muhingo kama mwanahabari, bali kama miongoni mwa wahariri watano waanzilishi wa jukwaa hili," amesema Kwayu.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe ambaye ni mwanahabari kitaaluma, amesema pamoja na mengi mazuri aliyofanya Muhingo atamkumbuka kwa kumfungulia njia ya utendaji katika wilaya hiyo. Muhingo aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni.

Amesema atayaishi yale aliyoyaamini Muhingo ikiwemo utendaji wa kazi uliotukuka.

"Muhingo alikuwa mwalimu, kaka na kiongozi. Wananchi wa Handeni wameupokea kwa masikitiko msiba huu," amesema Gondwe.

Jane Mihanji, makamu mwenyekiti wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania amesema Muhingo amemaliza kazi aliyotumwa duniani, hivyo jukumu kwa waliobaki ni kuyaishi aliyoyatenda.

Mhariri Mtendaji wa kampuni ya New Habari, Absalom Kibanda amesema kuondokewa na Muhingo ni pigo kwa tasnia ya habari.

Amesema mbali ya kumfahamu katika habari, pia ni zaidi ya ndugu yake na kwamba, mazishi hayo ni furaha kwa sababu Muhingo alijiandaa kulala milele.

"Mara nyingi nikiwa nyumbani kwake, pembeni mwa kitanda chake pale Hospitali ya Aga Khan alikuwa akimsubiri mkewe aondoke na kuniambia nimechoka nataka kupumzika," amesema Kibanda.                      

Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe amesema msiba huo ni pigo kwa wanahabari wote.

Amesema alimfahamu Muhingo tangu kijijini kwao Kyela ambako alikuwa akienda kumsalimia kaka yake aliyekuwa daktari wa zahanati ya kwanza.

"Nimemfahamu siku nyingi, naelewa utendaji wake ni pigo kwa tasnia na Taifa kwa jumla," amesema.